LOS ANGELES: BAADA ya kuibua minong’ono na kuvutia maoni mengi, Mwanamuziki Miley Cyrus, ambaye ana umri wa miaka 33, amethibitisha rasmi kuwa anachumbiwa na Maxx Morando, mchezaji wa bendi ya Liily, baada ya miaka minne ya kuwa wapenzi.
Habari hii imethibitishwa na tovuti kadhaa maarufu kama Page Six na People za nchini Marekani.
Miley na Maxx walihudhuria uzinduzi wa ‘Avatar: Fire and Ash’ uliofanyika wikienda hii katika ukumbi wa Dolby Theatre, Hollywood, ambapo walikuwa wakipiga picha pamoja kwenye kapeti jekundu na kuzua minong’ono kwa wanaowafahamu huku wakihoji hatma yao.
Miley alionesha pete yake ya almasi aliyovaa kwenye kidole cha pete cha mkono wa kushoto, ikionekana wazi kwenye kila picha waliopiga.
Baadae, Miley alithibitisha habari hiyo kwa gazeti la People, akisema kuwa ana furaha sana katika hatua hii mpya ya maisha yake.
Alipoulizwa kuhusu uchumba wake, alisema “Nimefurahi sana na hili. Hii ni hatua kubwa sana kwangu, na nimekuwa nikijaribu kulinda faragha yetu. Nimefurahi kuwa na chaguo zaidi na kuwa na uwezo wa kuamua nini cha kushiriki, na umri wangu umenisaidia kuwa na uangalizi zaidi juu ya mambo ninayoyasema na kuyashiriki.”
Miley pia alielezea uhusiano wao kwa kuufananisha na mada za filamu ya ‘Avatar’, akisema filamu hiyo ni “kuhusu upendo, ustahimilivu wa familia, na kuunganishwa tena, naliona kuwa ni jambo la kufaa na kuendana na hali yangu ya sasa maishani.”
Kulingana na taarifa za Deux Moi, Miley alionekana akivaa pete hiyo kuanzia katikati ya Novemba mwaka huu, Pete hiyo pia ilionekana kwenye picha za chakula cha jioni cha siku ya kuzaliwa kwake mwishoni mwa mwezi huo.
Francesca Simons, msemaji wa mbunifu wa vito, Jacquie Aiche, alithibitisha kuwa Jacquie ndiye alitengeneza pete hiyo, ambayo ina jiwe kubwa la aina ya cushion lililowekwa kwenye pete nene ya dhahabu ya 14 karat.
Miley na Maxx walikuwa wa kwanza kuonekana kuwa wapenzi rasmi mnamo Desemba 2021, waliposhikiana na kuonekana wakipendekeza uhusiano wao kwenye picha za nyuma ya jukwaa wakati wa tamasha la likizo la Miley, ‘Miley’s New Year’s Eve Party’, huko Miami. Mnamo Aprili 2022, waliimarisha uhusiano wao kwa kuonekana wakipiga busu wakitembea kwenye mitaa ya West Hollywood.
Miley awali alikuwa ameolewa na mchezaji Liam Hemsworth kutoka Desemba 2018 hadi Agosti 2019, lakini baada ya talaka, sasa ameonesha wazi kuwa ana mpenzi mpya ambaye ni Maxx Morando.
The post Miley Cyrus achumbiwa na Maxx Morando first appeared on SpotiLEO.



