BARCELONA: vinara wa LaLiga FC Barcelona, wamethinitisha kuwa Kiungo wao Dani Olmo, atakosekana kwa takribani mwezi mmoja baada ya kuvunjika bega lake la kushoto.
Taarifa ya Barcelona imesema:
“Olmo amepata jeraha la kuvunjika bega lake la kushoto wakati wa mchezo dhidi ya Atletico Madrid jana. Baada ya vipimo kufanyika, matibabu yasiyo ya upasuaji yamechaguliwa. Muda wa makadirio ya kurejea ni mwezi mmoja.”
Olmo alipata jeraha hilo alipoanguka wakati akifunga bao la pili kati ya matatu kwenye ushindi wa 3-1 dhidi ya Atletico Madrid Jumanne usiku, ushindi uliowapeleka Barca kileleni mwa LaLiga kwa tofauti ya pointi nne.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Hispania, mwenye umri wa miaka 27, amekuwa akikumbwa na misururu ya majeraha tangu alipojiunga na miamba hao wa Catalonia mwaka 2024 akitokea RB Leipzig.
Olmo sasa anaingia kwenye orodha ndefu ya majeruhi wa Barca, akiwemo Fermin Lopez, Gavi, na kipa Marc-Andre ter Stegen, wakati klabu hiyo ikijiandaa kwa mchezo muhimu wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Eintracht Frankfurt wiki ijayo
The post Olmo nje mwezi mmoja first appeared on SpotiLEO.



