KLABU ya Simba, jana Desemba 2, 2025 imetangaza kufikia makubaliano ya kusitisha mkataba na Meneja Mkuu, Dimitar Pantev pamoja na wasaidizi wake wawili.
Uamuzi huo wa Simba umekuja baada ya Pantev kudumu klabuni hapo kwa takribani siku 61 sawa na miezi miwili pekee, kutokana na kutambulishwa Ijumaa ya Oktoba 3, 2025, kisha mkataba wake kusitishwa Jumanne ya Desemba 2, 2025
Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba Desemba 2, 2025, imesema: “Uongozi wa klabu ya Simba umefikia makubaliano ya pande zote mbili ya kusitisha mkataba na Meneja Mkuu, Dimitar Pantev pamoja na Wasaidizi wake wawili.
“Kwa sasa kikosi kitabaki chini ya Kocha Selemani Matola wakati mchakato wa kutafuta Kocha mwingine unaendelea.”
Pantev aliyetua Simba akitokea Gaborone United ya Botswana sambamba na msaidizi wake, Boyko Simeonev, ameiongoza timu hiyo kucheza mechi tano za mashindano tofauti, ikishinda mbili, sare moja na kupoteza mbili.
Inaelezwa kwamba, matokeo yasiyoridhisha ndiyo yamechangia Pantev kusitishwa mkataba wake kwani Simba imepoteza mechi zote mbili za hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ikianza kufungwa nyumbani bao 1-0 dhidi ya Petro Atletico, kisha ikachapwa ugenini mabao 2-1 na Stade Malien.
Katika Ligi ya Mabingwa, pia Simba chini ya Pantev ilishinda mechi moja ugenini dhidi ya Nsingizini Hotspurs kwa mabao 3-0 ikiwa ni hatua ya pili kuwania kufuzu makundi. Pia aliiongoza kushinda 2-1 ugenini ikiwa ni mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya JKT Tanzania.
Rekodi zinaonyesha, Pantev kwa mwaka huu 2025 pekee, amezifundisha timu mbili tofauti akianza na Gaborone United aliyotua Januari 23, akadumu kwa muda wa miezi minane (siku 254) na Simba aliyodumu kwa miezi miwili (siku 61).
Pantev anaondoka Simba ikiwa ni siku mbili kabla ya kikosi hicho kucheza dhidi ya Mbeya City kwenye Ligi Kuu Bara, huku Jumapili ya Desemba 7, 2025 kikiwa na mechi nyingine ya Mzizima Dabi dhidi ya Azam katika mwendelezo wa ligi hiyo.
The post PAMOJA NA MBWEMBWE ZOTEE…PANTEV KALIPWA MISHAHARA 2 TU…KISHA KATIMULIWA SIMBA 😅😅… appeared first on Soka La Bongo.



