LONDON: KOCHA Nuno Espírito Santo wa West Ham United, amesema kiungo wa klabu hiyo Lucas Paquetá, anapitia kipindi kigumu na amesikitishwa sana na kutolewa kwake nje kwa kadi nyekundu katika kichapo chao cha mabao 2-0 dhidi ya Liverpool Jumapili.
Paquetá mwenye umri wa miaka 28, alipewa kadi mbili za njano kwa kupingana na mwamuzi (dissent) ndani ya sekunde 60, zikiwa zimebaki chini ya dakika 10 kumaliza mchezo. Licha ya jitihada za wachezaji wenzake kumbembeleza, mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil aliendelea kumshambulia kwa maneno mwamuzi Darren England, ndipo alipotolewa nje.
Baada ya mchezo, Paquetá alilishambulia pia Shirikisho la Soka England (FA), akilituhumu kushindwa kumpa msaada wa kisaikolojia wakati wa uchunguzi wa tuhuma za upangaji matokeo (spot-fixing). Licha ya kuomba radhi kwa wachezaji wenzake na mashabiki, alidai kitendo chake hakikustahili kadi nyekundu.
Mwezi Julai, FA ilitupilia mbali mashtaka manne ya spot-fixing yaliyokuwa yakimkabili baada ya uchunguzi wa muda mrefu. Paquetá, ambaye alikuwa anakabiliwa na uwezekano wa kufungiwa maisha, alikana tuhuma hizo tangu mwanzo.

“Nimezungumza na Lucas na ameomba radhi kwa wachezaji wenzake. Hajisikii vizuri. Anasumbuka, amekata tamaa na amehuzunika, lakini anatambua kosa alilofanya na anataka kuendelea mbele. Watu mara nyingi hawaelewi matatizo ambayo wachezaji hupitia, lakini Lucas atavuka hili.”
“Nadhani uchunguzi ulimuathiri, lakini yuko tayari kusonga mbele na kuyaweka pembeni yote ili aendelee kucheza soka kama kawaida. Tumefanya mazungumzo mazuri. Kikosi kinamuunga mkono Lucas.” – Nuno amesema.
Paquetá alijiunga na West Ham akitokea Olympique Lyonnais mwaka 2022 na ana mkataba hadi mwaka 2027. Licha ya fununu kuhusu mustakabali wake, Nuno amesisitiza kuwa kiungo huyo ana furaha ndani ya kikosi hicho cha Mashariki mwa London.
The post “Paquetá anapitia magumu” – Nuno first appeared on SpotiLEO.






