LONDON: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta, amekosoa ratiba ya Ligi Kuu England baada ya kiungo Declan Rice na beki Cristhian Mosquera kuwa wachezaji wa hivi karibuni kuongezeka kwenye orodha ya majeruhi wa klabu hiyo wakati wa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Brentford Jumatano usiku.
Arsenal tayari inakabiliwa na upungufu mkubwa kikosini, ikiwakosa mabeki tegemeo William Saliba na Gabriel Magalhães, pamoja na washambuliaji Kai Havertz na Leandro Trossard.
Mosquera alilazimika kutolewa muda mfupi kabla ya kipindi cha kwanza kutamatika kutokana na kile Arteta alichosema ni majeraha ya goti au kifundo cha mguu, huku Rice akitolewa dakika ya 83 baada ya kupata tatizo la misuli ya kifundo cha mguu (calf).

“Ni wazi hizi si habari njema kwetu. Declan alilazimika kutoka. Tutajua kesho tatizo lake ni nini, Mosquera naye yuko nje. Tayari tunawakosa Gabi na Willy. Inabidi tujiandae na kukabiliana na hali hii. Hilo limekuwa jambo linalojirudia msimu huu.”
Kuhusu Rice, Arteta alisema: “Hawezi kuendelea kucheza. Anaweza kutembea, lakini kucheza hapana. Tutangoja vipimo vya kesho.”
Arsenal inatarajiwa kuvaana na Aston Villa wanaong’ara msimu huu Jumamosi kabla ya kuelekea Ubelgiji kumenyana na Club Brugge katika Ligi ya Mabingwa tarehe 10 Desemba.

The Gunners, wanaoongoza msimamo wa Champions League, walirejesha pengo la pointi tano kileleni mwa Premier League kupitia bao la mapema la Mikel Merino na jingine la Bukayo Saka dakika za mwisho dhidi ya Brentford.
Arteta aliongeza kulalamika kuhusu ratiba ngumu inayowakabili:
“Sasa tunacheza Jumatano usiku, halafu tunatakiwa kucheza Jumamosi asubuhi pia. Tunaweza kucheza, lakini tafadhali tuongezeeni muda kidogo tu wa kupumzika ili kuboresha ustawi wa wachezaji.”
“Tupeni siku moja zaidi, hususan timu zinazocheza mara kwa mara Ulaya. Hii ni kwa manufaa ya wote. Hatujawahi kuwa na ratiba ngumu kiasi hiki katika kila ngazi Premier League, mashindano ya kimataifa, kila mahali. Wachezaji sio mashine.”
The post Arteta alia na ratiba EPL first appeared on SpotiLEO.








