CAXIAS DO SUL: KIUNGO mshambuliaji wa klabu ya Santos Neymar Jr ameonesha uzalendo wa hali ya juu kwa klabu hiyo iliyomlea baada ya kucheza akiwa na jeraha la goti na kufanikiwa kufunga hat-trick iliyoiinua klabu yake hiyo ya utotoni, kutoka kwenye hatari ya kushuka daraja katika Ligi Kuu ya Brazil, Serie A.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33, aliyewahi kuichezea Barcelona na Paris St Germain, alifunga mabao matatu ndani ya dakika 17 pekee na kuipa Santos ushindi wa 3-0 dhidi ya Juventude Jumatano usiku, ushindi uliowapeleka pointi mbili juu ya eneo la kushuka daraja huku wakibakiza mechi moja.
Neymar amekuwa akikumbwa na majeraha kwa muda mrefu na hajaiwakilisha timu ya taifa ya Brazil tangu Oktoba 2023.
Kocha wa Brazil, Carlo Ancelotti, alisema mwezi Oktoba kwamba Neymar bado yupo kwenye mipango yake kuelekea Kombe la Dunia la mwakani, lakini mshambuliaji huyo anatakiwa kurejesha utimamu wake wa mwili.
Neymar amefunga mabao matano na kutoa pasi moja ya goli katika mechi tatu zilizopita, akisaidia Santos kukusanya pointi saba na kupanda hadi nafasi ya 14 kwenye msimamo. Watakuwa wenyeji wa Cruzeiro Jumapili katika mechi ya mwisho ya msimu.
The post Neymar Jr apiga ‘hat-tick’ akiwa majeruhi first appeared on SpotiLEO.





