DAR ES SALAAM: MABINGWA watetezi Yanga SC wameendelea kujiimarisha kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fountain Gate, mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa KMC, Dar es Salaam.
Mabao ya Yanga yalifungwa na Prince Dube dakika ya 28 kwa mkwaju wa penalti na Pacome Zouazou dakika ya 80, ushindi uliowasukuma juu kutoka nafasi ya tano hadi ya tatu baada ya kufikisha pointi 13.
Bao la kwanza lilitokana na shuti la hatari lililoishia kugonga mkono wa beki wa Fountain Gate ndani ya eneo la 18, hali iliyompa Dube nafasi ya kufungua ukurasa wa mabao kwa utulivu kupitia mkwaju wa penalti.
Licha ya Fountain Gate kujaribu kurejea mchezoni, Yanga walionesha ubora wao hadi dakika za mwisho, ambapo Zouazou aliyeingia kipindi cha pili alimalizia kazi ya Duke Abuya kwa bao la pili dakika 10 kabla ya mchezo kumalizika.
Ushindi huo unaendelea kuiweka Yanga kwenye kasi nzuri ya kuwania nafasi za juu huku ikionesha uimara katika safu ya ulinzi na ushambuliaji.
The post Yanga yaifunga 2-0 Fountain Gate first appeared on SpotiLEO.





