DAR ES SALAAM: MSANII wa Bongo Fleva anayeishi nchini Afrika Kusini, Maulidi Lukwale ‘Mau Music’, ameendelea kutikisa anga la muziki punde tu baada ya kuachia albamu yake fupi (EP) iitwayo Still Mshua.
Kwa muda mrefu Mau Music amekuwa mstari wa mbele kutetea na kutangaza muziki wa Bongo Fleva nchini Afrika Kusini, akiuonyesha kwa mchanganyiko wa ladha na lugha mbalimbali za huko na kujipatia umaarufu kama MswaZulu.
Akizungumza na Spoti Leo kuhusu kazi hiyo mpya, Mau Music amesema Still Mshua imebeba ngoma kali kadhaa zikiwamo Sawa, Million Monsters, Oyoyo, No One, Lukelu, Champion, Swali na Iqolo.
“Sasa hivi EP inapatikana kwenye majukwaa yote ya muziki duniani. Nawashukuru wasanii wakubwa kama Jay Moe, Mr Blue, Music Holiq, Prince Papito, G Funk SA, Dinkii, Kamungu, Papi na Dan Cruz kwa kuipamba Still Mshua.
Naamni hii ni EP bora kabisa kwa mwaka huu kwa sababu namba zake zinaniridhisha, na ninaendelea kuisukuma iwafikie mashabiki wengi Afrika na duniani kote,” amesema Mau Music.
Kwa mujibu wa msanii huyo, ujio wa Still Mshua unatarajiwa kuendelea kuipeperusha bendera ya Bongo Fleva kimataifa kupitia ubunifu na ushirikiano aliofanya na wasanii kutoka mataifa mbalimbali.
The post Mau Music atamba na EP yake mpya Still Mshua first appeared on SpotiLEO.






