MANCHESTER: NAHODHA wa zamani wa Manchester United, Roy Keane, amesema kikosi cha sasa cha United kinaonekana kuwa na hofu na hakikuwa na ukali unaohitajika ili kupata pointi tatu, baada ya kuruhusu bao la dakika za mwisho na kulazimishwa sare ya 1-1 na West Ham United Alhamisi usiku Uwanjani Old Trafford.
United walikosa nafasi ya kupanda hadi nafasi ya tano licha ya kujipatia bao la kuongoza kupitia Diogo Dalot, kabla Soungoutou Magassa wa West Ham kusawazisha dakika ya 83.
Hii ni mara ya tatu katika mechi tano zilizopita kwa United kushindwa kuupata ushindi licha ya kupata bao kwanza, hali inayowaacha katika nafasi ya nane wakiwa na pointi 22 pointi 11 nyuma ya vinara Arsenal.

“Kila mara ninapoangalia timu hii (United), wananikosesha tumaini. Hawamalizi mechi, hawana ukali wa kumaliza kazi. Katika mechi zao tatu au nne zilizopita wamekuwa duni sana. Nafasi ya kupata ushindi walikuwa nayo, lakini walionekana kana kwamba wanaogopa.” – Amezungumza Roy Keane katika mahojiano na Sky Sports.
Dalot aliyefunga bao la United alisema kikosi chao kilipata wasiwasi ulioathiri mchezo baada ya bao lao, kauli ambayo Keane aliikosoa vikali.
“Ukicheza Manchester United ni lazima ushughulikie shinikizo la ndani na nje ya uwanja. Kama wachezaji wanakuwa na wasiwasi, basi unajiuliza wanachokihofia ni nini? West Ham kwa nini iwe tishio kiasi hicho? Wamefunga mabao mawili dhidi ya Palace kisha wakayalinda kama timu ya vijiweni.”
Manchester United wanatarajiwa kuvaana na Wolves walio mkiani wa msimamo wa EPL Jumatatu.
The post Roy Keane aikosoa vikali Man U first appeared on SpotiLEO.








