MSHAMBULIAJI wa Simba SC Mohamed Bajaber amefunguka baada ya kufunga bao lake la kwanza tangu ajiunge na Wekundu wa Msimbazi, akisema alikuwa akipita kwenye kipindi kigumu cha kukosa nafasi kutokana na majeraha yaliyomuweka nje kwa muda mrefu.
Mchezaji huyo, aliyesajiliwa msimu huu akitokea Polisi Kenya, hakuweza kuanza kuitumikia Simba mapema kutokana na changamoto za kiafya zilizomuweka nje na kumlazimu kushuhudia wenzake wakicheza huku yeye akiwa benchi.
Amesema muda wote alipoendelea kukaa nje bila uhakika wa ni lini angepata nafasi ya kucheza ulikuwa mgumu sana kwake kama mchezaji mpya aliyekuwa na shauku ya kuonesha uwezo wake.
Katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mbeya City, mshambulizi huyo aliingia kipindi cha pili na kufunga bao la tatu lililoweka muhuri ushindi wa timu yake bao ambalo lilikuja na hisia kubwa kwake.
Alionekana mwenye furaha isiyofichika aliposhangilia bao hilo, akisema limempa nguvu na imani mpya ya kupambana zaidi.
“Nimepitia wakati mgumu sana, kuona wenzangu wanacheza mimi nikiwa nje haikuwa rahisi. Lakini namshukuru Mungu, leo nimepata nafasi na nimefunga. Nikipewa nafasi zaidi, nitaendelea kufunga na kusaidia timu,” alisema.
Mashabiki wa Simba wamepokea kwa furaha kurejea kwa mchezaji huyo kwani walikuwa wakimshangilia na hat baada ya mechi walimtunza fedha kuonesha namna wanaamini anaweza kuwa miongoni mwa wachezaji muhimu.
The post BAADA YA KUFUNGA GOLI 1 LA LIGI….BAJABER AFUNGUKA MAGUMU YA SIMBA… appeared first on Soka La Bongo.







