KOCHA wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi ameiangalia timu hiyo kupitia mechi mbili za awali za Kundi B za Ligi ya Mabingwa Afrika na kujikuta akifurahi, kisha akawapa ushauri wa mambo akisema kama wakitulia wanatinga robo fainali.
Katika mechi hizo mbili, Yanga ilianza na ushindi wa bao 1-0 mbele ya AS FAR Rabat ya Morocco kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar kisha kwenda kutoka suluhu dhidi ya JS Kabylie ya Algeria na sasa kulingana pointi na Al Ahly ya Misri kila moja ikiwa na pointi nne.
Akizungumza akiwa kwake Ubelgiji, Nabi amesema alivutiwa na namna Yanga ilivyocheza mechji mbili za kwanza akidai imeonyesha kiwango kikubwa kiufundi dhidi ya timu mbili kubwa za Afrika Kaskazini.
Nabi amesema namna Yanga ilivyoonyesha kiwango katika mechi hizo mbili, kimetosha kubadilisha sura ya kundi hilo na kwamba lolote linaweza kutokea kwa mwabingwa hao kuweza kufuzu kufika hatua ya robo fainali.
“Kila mmoja aliona ni kama Yanga imeangukia kundi ambalo haitaweza kufanya kitu na kufika robo fainali lakini hizi mechi mbili tu ilizocheza zimebadili kila kitu na kuona namna Yanga nayo inaweza kupata nafasi ya kwenda mbali,” amesema Nabi na kuongeza;
“Nimefanya kazi Yanga na AS Far Rabat sio rahisi kushinda mbele ya Rabat lakini imewezekana, kitu ambacho Yanga ilikifanya ni kuwa bora wakati wana mpira na wakati hawana mpira, ukiangalia timu zote mbili zilipata ushindani wa ubora wa Yanga.”
Aidha Nabi amesema Yanga kama itapata pointi moja au tatu katika mechi mbili zijazo dhidi ya Al Ahly hatua hiyo itazidi kuongeza uhakika wa kufika robo fainali, huku akipongeza mipango ya kocha wa timu hiyo ya Jangwani, Pedro Goncalves.
Yanga itasafiri kuifuata Al Ahly kati ya Januari 23-25 mechi zitakazopigwa Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, kisha timu hizo kurudiana wiki moja baadaaye kati ya Januari 30 na Februari 01 kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar.
“Kitu muhimu ambacho Yanga inatakiwa kujipanga nacho sasa ni namna watakavyoingia kuicheza mechi mbili zijazo dhidi ya Al Ahly, kama watapambana kupata pointi kwenye mechi hizo nadhani wataongeza zaidi uhakika kwamba wanawesza kufika robo fainali,” amesema Nabi aliyeifikia timu hiyo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikipoteza kwa faida ya bao la ugenini dhidi ya USM Alger ya Algeria.
“Wanachotakiwa kufanya ni kuendelea kuimarika kwenye ubora, unaposhinda mbele ya AS FAR Rabat na kupata sare kwa Kabylie wachezaji wako kuna ujasiri wanaupata, nimefurahi kuona kocha wao ameonyesha ubora kwa timu kujiamini hata ikiwa ugenini,” aliongeza Nabi.
The post PAMOJA NA KUANZA VYEMA CAF….NABI ATIA NENO YANGA…AFUNGUKA UDHAIFU NA UBORA …. appeared first on Soka La Bongo.






