MABOSI wa Simba wamefurahishwa na kazi iliyofanywa na kocha Seleman Matola baada ya kuiongoza timu hiyo kupata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mbeya City, lakini hiyo haijawazuia kuendelea na mchakato wa kusaka kocha mpya ikielezwa kwa sasa wametua Barcelona, Hispania.
Simba inasaka kocha mpya baada ya kumtema Dimitar Pantev aliyetambulishwa kama meneja akiitumikia kwa siku 61 na sasa inadaiwa ipo katika mazungumzo na kocha mzawa wa Barcelona aliyeinoa Petro Atletico ya Angola.
Kocha huyo ni Antonio ‘Toni’ Cosano Cantos aliyezaliwa Machi 28, 1977 huko Barcelona akiwa na umri wa miaka 48 anayedaiwa ameanza mazungumzo na Simba ili kama mambo yataenda fresh, basi kabla ya mechi za Ligi Kuu na zile za CAF atue Msimbazi.
Taarifa za kuaminika kutoka ndani ya Simba zinadai Toni Casano ni kati ya makocha waliotuma wasifu kuomba kazi Msimbazi na mabosi wamemuelewa na sasa wanampigia hesabu kumshusha ili achukue nafasi inayokaimiwa na Matola aliyekuwa kocha mkuu chini Pantev.
“Mchakato wa kocha upo pazuri licha ya majina kuwa mengi, lakini kuna jamaa mmoja aliwahi kuinoa Petro Luanda mzaliwa wa Barcelona ndiye anayepigiwa hesabu akiwa katika mazungumzo na vigogo, mmoja aliyewahi kuwa mwenyekiti wa klabu,” kilisema chanzo hicho.
“Ni kocha kijana kama ilivyokuwa kwa Fadlu Davids na hata Pantev, lakini kubwa ni aina ya soka lake linaendana na falsafa ya Simba, kwani akiwa Petro alifanya makubwa ikiwamo kuingiza timu makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2020-2021.
Kocha huyo mwenye Leseni ya UEFA Pro ambayo inalinda na Leseni A CAF mbali na kuifundisha Petro du Luanda, lakini amewahi kuinoa Moghreb Atlético Tétouan ya Morocco mbali na timu kadhaa za vijana wakati akiwa Hispania kati ya mwaka 2006-2016.
Alitua Petro 2017 na kuinoa timu ya vijana ya klabu hiyo ya Angola kabla ya kupewa timu kubwa 2019 na kuiwezesha kuongoza msimamo wa Girabola kabla ya Ligi kusimama kwa tatizo la Uviko-19 hadi 2021 alipondoka na kwenda Morocco.
“Hata hivyo, mchakato unaendelea na taarifa rasmi zitatolewa na mabosi wakuu, ila hadi sasa hesabu za Simba zipo kwa Toni Casano,” chanzo hicho kilisisitiza.
MASTAA NA MATOLA
Hata hivyo, mara baada ya pambano la juzi mbele ya Mbeya City baadhi ya mastaa wa Simba wameonyeshwa kufurahishwa na Matola na kuutaka uongozi kama inawezekana wampe tu jumla kocha huyo timu hiyo.
Kauli ya mastaa hao, iliungwa mkono pia na mfadhili wa zamani wa Simba, Azim Dewji aliyesema umefika muda wa Matola kuaminiwa, kwani uzoefu alionao nao na vigezo vinambeba kwa sasa.
Azim amesema kwa sasa wanachotaka kama viongozi na mashabiki ni Simba kurejea katika ubora uliozoleka.
“Furaha yetu wanasimba ni pale malengo yetu yanapotimia kuchukua pointi tatu katika michezo yote ya Ligi na Kimataifa, sio swala la kuwa na kocha mweupe. Kama kutakuwa na mazungumzo na kocha yeyote kwa sasa bado mapema ila ukweli ni kwamba, huu ni wakati sahihi wa Matola kupewa kijiti,” amesema Azim aliyeiwezesha Simba kucheza fainali ya kwanza ya Kombe la CAF 1993 enzi hizo akiwa mfadhili na timu ikifundishwa na Abdallah Kibadeni akisaidiana na Etienne Eshete aliyetokea Somalia na kupoteza mbele ya Stella Abidjan ya Ivory Coast kwa mabao 2-0.
Mbali na Azim, pia baadhi ya wachezaji wa Simba wakiwamo wazawa wanaocheza kikosi cha kwanza na wa kigeni wanaoanza, na mmoja wa mtokea benchi wamemtaka Matola.
Beki na nahodha wa timu hiyo, Shomary Kapombe amesema haoni kama kutakuwa na tatizo kwa Simba endapo Matola akipewa timu kutokana na muda aliokaa naye na wanamuona kuwa ni kocha anayejua mambo mengi na ataibeba timu.
Beki huyo amesema licha ya Matola muda wote kuwa kocha msaidizi, lakini kila anapokuwa anatoa maelekezo yanakuwa na faida kubwa kwa wachezaji wa timu hiyo kama ilivyokuwa juzi dhidi ya Mbeya City.
“Huenda viongozi wana wasiwasi, lakini Matola ni kocha mzuri tu tunayekaa naye tunajua umuhimu wake ni vile hatuwezi kutoka na kutoa maelekezo wakati kocha mkuu yupo, ila anajua sana kufundisha,” amesema.
“Ukiangalia kocha Fadlu Davids kidogo ndiye alikuwa anampa hata nafasi ya kusema kitu kwa kuwa alikuwa anamkubali ingawa muda mwingi alikuwa sana na yule msaidizi, lakini ukiangali huyu Pantev (Dimitar) ilikuwa kama anamuangalia Matola kama mpinzani wakati angeweza kumsaidia.”
Kiungo mzawa wa Simba (jina kapuni), amesema kama angekuwa na uwezo angeuomba uongozi umpe Matola timu jumla kwani ni mtu anayeijua kazi yake.
“Nadhani wewe umeifuatilia sana Simba, angalia kila makocha wakifukuzwa timu huachiwa Matola na amekuwa akipata matokeo mazuri? Mara nyingi tumekuwa tunashinda na sio kushinda tu tunaupiga mwingi,” amesema kiungo huyo akiungwa mkono na nyota wa kigeni anayecheza eneo la ushambuliaji aliyesema: “Nilianza kukata tamaa, lakini amekuwa akiniambia anaamini mimi nina kipaji cha kuisaidia timu wala nisionyeshe kitu kibaya wakati wangu wa kucheza utakuja na nitafunga na sasa huwezi amini nina furaha.”
The post WAKATI KAPOMBE AKIMTAKA MATOLA….KOCHA MUHISPANIA ANUKIA MSIMBAZI…. appeared first on Soka La Bongo.








