KUELEKEA mchezo wa leo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Msemaji wa Azam FC, Hashim Ibwe, ametoa tahadhari kwa Simba akisema kuwa licha ya timu yake kuingia kwenye mchezo huo ikiwa na matokeo mabaya, bado wana uwezo wa kusababisha kilio kwa wekundu wa Msimbazi.
Mtanange huo unaotarajiwa kuchezwa saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, unachukuliwa kama mmoja wa michezo yenye ushindani mkali wiki hii, huku Azam FC ikitarajiwa kukutana na upinzani mkubwa kutoka kwa Simba.
Ibwe amesema matokeo yasiyoridhisha katika michezo yao ya hivi karibuni yameifanya Azam kuonekana kama timu inayokuja kinyonge mbele ya Simba.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa hawatakuwa wanyonge ndani ya dimba hilo, bali wataingia kucheza kwa kujiamini na kufuata mbinu zao.
“Ni kweli tunaingia kinyonge kutokana na matokeo ya nyuma, lakini hatutaenda kwa uoga. Tunaenda kucheza mpira wetu wa kawaida,” amesema Ibwe.
Ameongeza kuwa licha ya changamoto walizokumbana nazo, Simba wanapaswa kuwa makini kwa sababu mechi kubwa haiamuliwi na historia, bali ubora wa siku husika na Azam wana uwezo wa kufanya maajabu.
“Simba isijiachie sana, maana tunaweza kushinda hapo. Timu kubwa lazima ishinde mechi kubwa, ikiwemo hii ya leo,” amesema Ibwe.
Msemaji huyo ameonyesha imani kubwa kwa kocha wao, Florent Ibenge, akisema ameleta mwelekeo mpya ndani ya kikosi hicho na anazidi kupambana kuhakikisha wanarejea katika mstari wa ushindani.
Hadi sasa, Azam FC inashika nafasi ya 14 ikiwa na alama sita baada ya michezo minne, huku Simba ikishika nafasi ya tano na alama 12 kabla ya mchezo wa leo.
The post HASHIM IBWE; SIMBA KUFANYWA VIBAYA MZIZIMA DERBY appeared first on Soka La Bongo.





