KIKOSI cha Yanga kinatarajiwa kushuka dimbani leo kukabiliana na Coastal Union katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, ambapo Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ali Kamwe, amesisitiza kuwa lengo lao kubwa ni kuondoka na alama tatu muhimu.
Kamwe amesema ushindi katika mchezo huo utawasaidia kuhitimisha mwaka 2025 wakiwa na rekodi chanya, jambo ambalo linaongeza hamasa kwa wachezaji na benchi la ufundi.
Akizungumza kuelekea mchezo huo unaotarajiwa kuanza saa 1:00 usiku, Kamwe alibainisha kuwa maandalizi ya timu yako katika kiwango bora, huku wachezaji wakiwa na morali ya juu na utayari wa kupambana ili kupata matokeo mazuri.
Ameeleza kuwa mchezo wa leo ni sehemu ya mkakati wao wa kuhakikisha kila mechi inakuwa fursa ya kuongeza pointi na kujiimarisha kwenye msimamo wa Ligi Kuu, hasa katika kipindi hiki ambacho ushindani umeongezeka na kila pointi ina thamani kubwa.
Kamwe amefafanua kuwa Yanga imejiwekea utaratibu wa kupambana kwa nguvu katika kila mchezo, ikiwemo huu dhidi ya Coastal Union, hakuna nafasi ya kupoteza umakini katika msimu huu wenye changamoto nyingi.
Amesema baada ya mchezo wa leo, ligi itasimama kwa takribani mwezi mmoja kupisha mashindano ya AFCON, klabu haitaki kwenda kwenye mapumziko ikiwa na matokeo yasiyoridhisha. Kwa sababu hiyo, wanahitaji ushindi ili kusimama kwenye “gia nzuri” kabla ya mapumziko hayo.
“Tumekuwa na michezo miwili ya karibuni tuliyocheza vizuri, tumepata ushindi dhidi ya Fountain Gate FC, na sasa tunahitaji alama tatu mbele ya Coastal Union ili tumalize mwaka kwa mafanikio,” amesema Kamwe.
Kamwe ameongeza kuwa kikosi cha Yanga kimeimarika zaidi baada ya kupita kwenye kipindi kigumu cha majeraha na uchovu. Kwa sasa wachezaji wengi wamepona na kurejea kwenye ubora wao, hali iliyoongeza nguvu na ushindani ndani ya timu.
Kurejea kwa wachezaji waliokuwa majeruhi kumetoa mwanga mpya kwa benchi la ufundi, ambalo sasa lina chaguo pana la kupanga kikosi imara kitakachoweza kuisaidia timu kupata matokeo katika michezo ijayo.
Kwa ujumla, Yanga inaingia uwanjani ikiwa na dhamira ya kuendeleza kasi ya ushindi na kujihakikishia pointi tatu muhimu kabla ya ligi kusimama na mwaka kumalizika.
The post YANGA KUFUNGA MWAKA NA REKODI YA AJABU; ALI KAMWE appeared first on Soka La Bongo.






