MSHAMBULIAJI wa Yanga, Prince Dube, ameibuka kuwa shujaa wa kikosi hicho baada ya kufunga bao pekee dakika ya 89 na kuiwezesha timu yake kuvuna alama tatu muhimu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Yanga waliingia uwanjani wakijua umuhimu wa ushindi huo, kwa mara nyingine tena wakaonyesha ukubwa wao ndani ya ardhi ya nyumbani kwa Coastal Union kwa kutawala mpira na kutengeneza nafasi nyingi za hatari.
Prince Dube, aliyeanza msimu kwa changamoto ya ukame wa mabao, ameongeza bao lake la pili msimu huu, akithibitisha kurejea kwenye ubora na kuonesha dalili za kuwa mfungaji tegemeo wa Wananchi katika mechi zijazo.
Kipindi cha kwanza kilimalizika bila timu yoyote kufanikiwa kuona lango la mwenzake, licha ya jitihada za makocha wote wawili kuhakikisha wanapata mwanya wa kuhitaji matokeo mapema. Safu za ulinzi za timu zote zilionekana imara na makini.
Mara baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, Yanga waliongeza kasi ya mchezo na kutafuta bao la kuongoza, huku Coastal Union wakionekana kujilinda zaidi ili kuzuia mashambulizi ya wageni wao.
Dakika ya 71, Yanga walikaribia kupata bao kupitia kwa Dube, lakini kipa wa Coastal Union, Wilbol Maseke, aliwazuia kwa umahiri mkubwa baada ya kuutoa mpira uliokuwa ukielekea wavuni, na kuendelea kuiokoa timu yake.
Hata hivyo, juhudi hizo hazikutosha kuzuia nguvu ya mashambulizi ya Yanga, katika dakika za jioni, Dube akapokea pasi safi na kumalizia vyema kwa kumpiga Maseke na kuwanyanyua mashabiki wa Yanga waliokuwa Jamhuri.
Kwa ushindi huo, Yanga wamejijengea mazingira mazuri zaidi katika mbio za kutetea taji lao la Ligi Kuu Tanzania Bara, wakionyesha dhamira ya kutaka kulitwaa tena kwa msimu mwingine mfululizo.
The post PRINCE DUBE ATIKISA DODOMA KIVINGINE appeared first on Soka La Bongo.






