KOCHA wa Viungo na Utimamu wa Mwili wa Simba, Riedoh Bierden, ameweka wazi changamoto ambazo kikosi hicho kinakabiliana nazo, akisisitiza kuwa ndizo zimechangia kuporomoka kwa kiwango na kupoteza mchezo dhidi ya Azam FC katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba ilijikuta ikipoteza mchezo wake wa kwanza wa msimu huu baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Azam FC, kwenye mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Matokeo hayo yalizua maswali mengi kutoka kwa mashabiki na wadau wa soka nchini.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Bierden amesema kikosi chao kinacheza kwa ubora mkubwa ndani ya dakika 90 lakini tatizo la kumalizia nafasi limekuwa likiwagharimu sana, jambo ambalo wanalipa kipaumbele katika kipindi hiki cha mapumziko.
“Simba tunacheza vizuri sana, lakini bado tuna changamoto chache katika eneo la umaliziaji. Nafasi tunapata, lakini hatuzitumii ipasavyo. Hata hivyo tunaamini kipindi hiki cha mapumziko tutakitumia kurekebisha mapungufu yetu,” amesema Bierden.
Kocha huyo ameongeza kuwa benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu Selemani Matola linafanya kazi kwa kushirikiana kuhakikisha wanairejesha Simba katika kiwango chake cha juu na kuendelea kupambana kwenye mbio za ubingwa.
Amesema wachezaji wanaendelea kupewa programu maalum za kuongeza umakini, nguvu na uimara wa mwili ili kuhakikisha wanarejea wakiwa bora zaidi pindi ligi itakaporejea kuendelea.
Kuhusu mabadiliko yanayoendelea ndani ya benchi la ufundi, Bierden amesisitiza kuwa hilo sio tatizo kubwa kama baadhi ya watu wanavyodhani, kwani mabadiliko ni sehemu ya mchezo na mara nyingi hutokea kwenye timu yoyote ile.
Ameongeza kuwa Simba inajipanga upya na haitakata tamaa, kwani inatambua bado ina nafasi kubwa ya kupambana na kurejea katika mstari wa ushindani, akiahidi mashabiki kwamba makosa yaliyopita hayatakuwa kikwazo katika michezo ijayo.
The post SIRI NZITO YAFICHUKA SIMBA KUFUNGWA NA…… appeared first on Soka La Bongo.





