MSHAMBULIAJI wa Wydad Casablanca wa Morocco, Seleman Mwalimu, anayekipiga Simba kwa mkopo, ameondolewa kwenye kikosi cha Taifa Stars kitakachoshiriki Fainali za AFCON 2025 nchini Morocco.
Hatua hiyo imekuja baada ya kocha mkuu, Miguel Gamondi, kufanya mchujo wa mwisho kabla ya kikosi kuelekea kwenye kambi maalum nchini Misri.
Awali, Mwalimu alikuwemo kwenye orodha ya wachezaji walioitwa kuiwania nafasi ya kuingia kikosi cha mwisho, na alishiriki mazoezi ya awali pamoja na wengine.
Hata hivyo, baada ya tathmini ya makocha, jina lake halikuonekana kwenye orodha ya wachezaji 28 waliochaguliwa kwenda Misri kuendelea na maandalizi.
Wachezaji waliothibitishwa kuingia kwenye kikosi hicho ni pamoja na golikipa Yakoub Suleiman (Simba SC), Hussein Masalanga (Singida BS), Zuberi Foba (Azam FC), Bakari Mwamnyeto (Young Africans), na Shomari Kapombe (Simba SC). Wengine ni Lusajo Mwaikenda (Azam FC) na Mohamed Hussein (Young Africans).
Aidha, safu ya ulinzi na kiungo inaendelea kukolezwa na nyota kama Nickson Kibabage (Singida BS), Alphonse Mabula (Shamakhi, Azerbaijan), Wilson Nangu (Simba SC), Novatus Dismas (Göztepe FC, Uturuki), Kelvin Nashon (Pamba Jiji) na Pascal Msindo (Azam FC).
Katika orodha hiyo pia wamo Ibrahim Abdulla (Young Africans), Haji Mnoga (Salford City, Uingereza), Dickson Job (Young Africans), Habibu Idd (Singida BS), Tarryn Allarakhia (Rochdale AFC, Uingereza) na Charles M’Mombwa (Floriana FC, Malta), ambao wote wameonyesha kiwango kizuri msimu huu.
Kwa upande wa washambuliaji, Gamondi amewaita Feisal Salum (Azam FC), Morice Abraham, Kibu Denis, Yusuph Kagoma (Simba SC), Abdul Suleiman, Iddi Suleiman (Azam FC), pamoja na nyota wanaocheza nje ya nchi; Mbwana Samatta (Le Havre AC, Ufaransa), Kelvin John (Aalborg BK, Denmark) na Simon Msuva (Al-Talaba, Iraq).
Tanzania imepangwa Kundi gumu linalojumuisha Tunisia, Uganda na Nigeria, hali inayowalazimu Stars kufanya maandalizi makubwa kuelekea AFCON 2025. Kikosi hicho sasa kinatarajiwa kupambana kuhakikisha kinafanya vizuri kwenye mashindano hayo makubwa ya barani Afrika.
The post SELEMANI MWALIMU AONDOLEWA KIKOSINI appeared first on Soka La Bongo.






