CAIRO: SHIRIKISHO la Soka nchini Misri (EFA) limethibitisha kuwa limetuma barua kwenda shirikisho la soka duniani FIFA likitaka kuzuia shughuli zozote zinazohusiana na maudhui ya wapenzi wa jinsia moja (LGBTQ+) wakati wa mchezo wa Kombe la Dunia kati ya timu ya taifa ya Misri na Iran utakaopigwa mjini Seattle Juni mwakani.
Kwa mujibu wa EFA, sherehe na matukio yaliyopangwa kuambatana na mchezo huo yanakinzana na mila na imani za mataifa yanayoshiriki, hasa ukizingatia kwamba Misri na Iran zina sheria kali dhidi ya watu wa mapenzi ya jiansia moja.
Mchezo huo uliopangwa Juni 26 umewepewa hadhi ya kuwa ‘Pride Match’ na waandaaji wa eneo hilo ukienda sambamba na maadhimisho ya Seattle Pride Weekend. Ripoti zinaeleza kuwa mipango ya shughuli hizo iliwekwa kabla ya droo ya makundi kuthibitisha pambano la Kundi G kati ya timu hizo mbili.
Katika barua yake kwa Katibu Mkuu wa FIFA, Mattias Grafstrom, EFA imesema inakataa kikamilifu kuwepo kwa matukio yoyote ya kuhamasisha matendo ya jamii ya LGBTQ+ wakati wa mchezo huo, ikionya kuwa hatua hiyo inaweza kuchochea ukinzani wa kitamaduni na kidini miongoni mwa mashabiki.

“Shughuli hizi zinakinzana moja kwa moja na maadili ya kitamaduni, kidini na kijamii ya ukanda huu, hususan katika jamii za Kiarabu na Kiislamu. Tunaomba FIFA ihakikishe kuwa mchezo unachezwa katika mazingira yanayozingatia michezo pekee bila maonesho yanayokiuka imani za mataifa yanayoshiriki,” – barua ya EFA imeeleza.
Shirikisho hilo limesisitiza kuwa ingawa FIFA inalenga kutoa mazingira ya heshima kwa mashabiki wote, ni muhimu kuepuka matukio ambayo yanaweza kusababisha mvutano au tafsiri potofu kati ya mashabiki wa Misri na Iran.
EFA imeitaja pia Ibara ya 4 ya Katiba ya FIFA, inayotaka mashindano yawe huru dhidi ya masuala ya kisiasa na kijamii, pamoja na kanuni za kinidhamu zinazozuia matamko yanayoweza kuleta migogoro au mvutano miongoni mwa mashabiki.
Nchini Iran, mahusiano ya jinsia moja yanaweza kuadhibiwa hadi kwa hukumu ya kifo, huku nchini Misri sheria za maadili zikitumika mara kwa mara kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watu hao.
The post Misri yaishika pabaya FIFA first appeared on SpotiLEO.








