BASEL: KLABU ya Aston Villa, iliyoko kwenye kiwango bora na ikija juu baada ya kuwachabanga vinara wa Ligi Kuu England Arsenal, inatarajiwa kuvaana na FC Basel kwenye UEFA Europa League (UEL) usiku wa leo Alhamisi.
Baada ya kuanza msimu kwa kusuasua, Villa imegeuka tishio na sasa ipo kwenye mwendelezo wa ushindi katika mechi saba mfululizo kwenye michuano yote, ikiwemo ushindi wa 2-1 dhidi ya Arsenal Jumamosi.
Mbali na kushika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu England, Villans wamefungana kileleni mwa msimamo wa Europa League wakiwa na pointi 12 sawa na Lyon na Midtjylland baada ya kushinda mechi nne kati ya tano.

“Kitu muhimu zaidi ni namna tunavyojenga timu, namna tunavyopiga hatua katika kila mashindano, na namna tunavyoimarika kisaikolojia katika kila kitu,” amesema kocha Unai Emery kuelekea mchezo huo utakaopigwa St. Jakob-Park, Basel. Emery tayari ametwaa taji la Europa League mara nne akiwa na Sevilla na Villarreal.
Sambamba na mchezo huo Lyon itakuwa nyumbani kuikaribisha Go Ahead Eagles kutoka Uholanzi, huku Midtjylland ikiwakaribisha Genk. Timu nane za juu baada ya michezo minane zitafuzu moja kwa moja hatua ya 16 bora mwezi Machi.
Katika nafasi za chini za msimamo wenye timu 36, Nice itakuwa ikisaka pointi zake za kwanza watakapokutana na Braga.
The post Aston Villa kuendeleza ubabe UEL leo? first appeared on SpotiLEO.







