PARIS: MTANGAZAJI maarufu wa redio na Jaji wa American Got Talent Howard Stern amejibu vikali madai ya Kim Kardashian kwamba alimshutumu kughushi tukio lake la wizi la mwaka 2016 mjini Paris.
Kim, mwenye miaka 45, aliwahi kushambuliwa na wanaume waliovamia chumba chake cha hoteli jijini Paris na kumshikilia kwa bunduki, wakimvua vito vyenye thamani ya takriban dola milioni 10. Hata hivyo watu hao wanane baadaye walikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa kuhusika na uporaji huo.
Katika toleo jipya la kipindi chake cha ‘The Kardashians’, Kim alirejea kumbukumbu hizo akisema kuwa aliathirika sana na madai kwamba Stern alinena hewani kuwa alibuni tukio hilo.
Lakini Stern amekana vikali madai hayo. Katika kipindi cha The Howard Stern Show cha Jumanne Decemba 09, 2025.
Akasema:“Kim anadai nilisema alighushi tukio lake la kuporwa Paris. Tulirudi tukacheki tulichosema, na ukweli ni kwamba hakuna jambo la uongo zaidi ya hilo. Tulichosema ni kwamba kulikuwa na watu waliokuwa wakidai hivyo, na hilo lilikuwa kweli.
Na tulisisitiza: Hatuamini kama ni uongo. Tuliamini alipitia jambo baya sana.”
Stern aliendelea kueleza kuwa katika mazungumzo yake ya 2016, yeye na mwenzake Robin Quivers walijadili tu habari za kipindi hicho bila kumtuhumu Kim moja kwa moja.
Katika rekodi ya zamani, Stern alisikika akisema:
“Kama kweli mwanamke huyu alivamiwa na wanaume wenye silaha, wakamtupa kwenye bafu na kumfunga, hilo ni jambo la kutisha sana.
Lakini kama lingekuwa maigizo, basi waliofanya hivyo wangestahili kwenda jela.”
Quivers alijibu: “Mimi sidhani kama ni maigizo”, naye Stern akakazia: “Mimi pia sisemi hivyo.”
Aliongeza kwa utani:
“Ni mara ya pekee familia ya Kardashian hawakuwa na kamera, halafu jambo la kufurahisha likatokea.”
Hata hivyo, katika kipindi cha karibuni cha ‘The Kardashians’, Kim alionekana akijiziba machozi akisema Stern aliwahi kufanya mzaha kwa kejeli kuhusu tukio hilo, akimwita mgonjwa na kudai alilitengeneza.
Akasema: “Alikuwa amesisitiza sana kwamba nimetunga. Nilishangaa, ‘Unawezaje kuwa na uhakika hivyo?’ Watu wanaokuamini wanasikiliza unachosema. Hilo limebaki moyoni mwangu.”
The post Howard Stern amjibu Kim Kardashian kauli ya wizi first appeared on SpotiLEO.







