LOS ANGELES: MUONGOZAJI filamu maarufu, James Cameron, amesema kuwa hatoitumia AI katika kazi zake za filamu na wala hana maslahi binafsi kutumia teknolojia hiyo.
Cameron, mwenye miaka 71, amesema hatotumia AI kuchukua nafasi ya ubunifu wa kibinadamu licha ya kuwa kiongozi mkubwa wa kutumia teknolojia za kisasa kwenye ulimwengu wa filamu zake.
Akizungumza kwenye Tamasha la Kimataifa la Filamu la Kisiwa cha Hainan, alisema:
“Sivutiwi kutumia zana ambazo zinatumia teknolojia kuchukua nafasi ya ubunifu wa binadamu. Inawezekana tukamzalisha muigizaji wa kimitambo kupitia AI, lakini mimi nisingefanya hivyo. Je, ni jambo linalotakiwa? Je, linaweza kuleta ule upekee unaotokana na uzoefu wa mwanadamu katika uandishi wa filamu na kwa waigizaji?”
Cameron amekiri kuwa AI inaweza kusaidia katika baadhi ya hatua za utengenezaji filamu, lakini akasisitiza kwamba studio zinapaswa kutumia teknolojia hiyo kwa uangalifu mkubwa.
Akaongeza:
“Tunaweza kuboresha mtiririko wa kazi, tukaifanya iwe rahisi na yenye ubunifu zaidi kupitia AI. Ndiyo, inawezekana. Lakini lazima tuendelee kuwa na viwango vya juu sana vya matumizi yake, kiethics, kimaadili na kiuhalisia.”
Cameroon aliyeongoza filamu ya Avatar amesisistiza kuwa AI haiwezi kufikia ubunifu wa kibinadamu.
“Ukimpa AI modeli iliyofundishwa kwa kila kitu, itaweza tu kutoa wastani. Inaweza kufanya ubora wa kawaida, lakini haiwezi kutoa kilicho cha kipekee kabisa. Haiwezi kuunda kitu ambacho hakijawahi kuonekana. Ukiiambia AI itengeneze kitu kinachofanana na ‘Avatar ‘sasa, inaweza kufanya hilo siku nzima.
Lakini ukimuuliza afanye hivyo kabla ‘Avatar’ haijatoka itashindwa kabisa. Mwishowe yote yanarudi kwa ubunifu wa binadamu.”
The post James Cameron aigomea Ai first appeared on SpotiLEO.







