DAR ES SALAAM: BONDIA wa kike kutoka Kambi ya Kivita Mburahati, Leila Macho, amemchimba mkwara mkali mpinzani wake Hidaya Zahoro wa Morogoro kuelekea pambano lao linalosubiriwa kwa hamu litakalofanyika Desemba 26, 2025 Dar es Salaam.
Akizungumza wakati akiendelea na mazoezi yake, Macho alisema Hidaya amekuwa akijifariji kwa “ndoto za mchana,” akisisitiza kuwa siku ya pambano ataonesha ubora wake kwa kutumia “ufundi na utaalamu wa hali ya juu.”
“Nimesikia anavyojifariji, lakini ukweli unabaki pale pale kipigo kitakuwepo. Mimi ni gari kubwa, halishikiki. Atapigwa kwa ufundi wa mchezo wenyewe,” alisema Macho kwa kujiamini.
Macho amesema maandalizi yake yamefikia hatua nzuri na amebakiza kusubiri siku yenyewe ili “kuacha ulingo ufanye mazungumzo.”
Wadau na mashabiki wa bondia huyo nao wameendelea kuonesha imani kubwa kwake, wakisema rekodi ya Hidaya haitamtetea siku ya pambano.
Nasra Msami, mmoja wa wadau wa mchezo huo, alisema Hidaya amepotoshwa na waliomtuma na kumtaka ajiandae kupokea “kipigo cha Dada Jambazi.”
Kwa upande wake, shabiki Ayubu Mwambo alisema Macho amekuwa na nguvu, wepesi na akili ya ulingoni, hivyo anaamini ushindi upo mikononi mwake.
Pambano hilo la Boxing Day litakusanya mabondia wengi wa ngumi kutoka mikoa mbalimbali wakiongozwa na pambano kuu la bondia nyota Hassan Mwakinyo na wengine wakiwemo Hamadi Furahisha vs Hanock Phiri (Malawi), Hassan Ndonga vs Ismail Boyka, Ally Ngwando vs Mussa Makuka, Issa Simba (Kahama) vs Wilson Phiri (Malawi) na Debora Mwenda vs Mariam Dick (Malawi)
Waandaaji wa pambano hilo Peak Time, wamesema lengo la onesho hilo ni kuinua kiwango cha ngumi za kulipwa nchini pamoja na kuwapa nafasi mabondia chipukizi kuonesha uwezo wao.
Mashabiki wanatarajia kuona pambano kali, hasa baada ya maneno ya kujiamini kutoka pande zote mbili kuelekea tukio hilo la mwisho wa mwaka.
The post Leila ‘Macho’ amchimba mkwara Hidaya Zahoro first appeared on SpotiLEO.







