MADRID: BAO la kinda Nico O’Reilly na penalti ya Erling Haaland vimeipa Manchester City ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Real Madrid katika mchezo wa kukata na shoka wa Ligi ya Mabingwa ulaya uliopigwa uwanjani Bernabéu Jumatano usiku.
Real Madrid walikuwa wa kwanza kutangulia kupitia Rodrygo dakika ya 28, akiimalizia kwa utulivu shambulizi la kushtukiza huku City ikionekana kuyumba kila mara Los Blancos waliposukuma mashambulizi katika dakika za mwanzo.
Lakini makosa ya Madrid yakawagharimu. Kwanza, kipa Thibaut Courtois aliteleza na kushindwa kudaka mpira rahisi wa kichwa kutoka kwa Josko Gvardiol, na O’Reilly kupiga kijishuti kilichojaa wavuni na kuisawazishia City dakika ya 35.

Dakika nane baadaye, beki Antonio Rüdiger alimwangusha Haaland ndani ya boksi alipokuwa akikimbilia mpira wa krosi, na baada ya VAR kumuita mwamuzi Clement Turpin atazame tukio, penalti ikatolewa. Haaland hakukosea, akipiga penalti safi upande wa kulia wa Courtois dakika ya 43.
Ushindi huo umeipandisha City hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi ya Mabingwa wakiwa na pointi 13 baada ya mechi sita, huku Madrid wakishuka hadi nafasi ya saba na pointi 12, wakipoteza kwa mara ya pili mfululizo katika mashindano yote.
Mashabiki wa Bernabéu hawakuificha hasira yao kwa kocha Xabi Alonso, wakimzomea muda mwingi wa mchezo huku Real Madrid ikiendeleza na mwenendo mbovu ikiwa na ushindi mara mbili tu katika mechi nane zilizopita.

“Haitoshi tunaondoka tukiwa na hasira. Tulikuwa na kipindi cha kwanza kizuri, tulitaka kuanza kwa nguvu, tukapata bao… lakini tunahitaji kuboresha,” Rodrygo ameiambia Movistar Plus.
Madrid waliikosa huduma ya wachezaji nane kutokana na majeraha, akiwemo mkali Kylian Mbappé, ambaye aliwekwa benchi baada ya kukosa mazoezi Jumanne. Hata hivyo, walikuwa na mwanzo mzuri, wakipata nafasi kupitia Vinícius Jr na Federico Valverde kabla ya Rodrygo kuifungua mechi na kumaliza ukame wa muda mrefu wa mabao.
City walionekana butu katika dakika 30 za kwanza, bila shuti lolote lililolenga lango, na wakiteswa zaidi upande wa kushoto ambapo Álvaro Carreras alikuwa akishirikiana vyema na Vinícius Jr. Lakini walifanya makosa yakawaua Madrid na Man City wakageuza mchezo kwa dakika chache tu.
Madrid walipata nafasi za kurejesha mchezo, huku chipukizi Endrick akipiga mwamba dakika za mwisho, lakini juhudi zao hazikutosha na kelele za kuzomea zikaongezeka kadri muda ulivyosonga

The post Man City yatamba Bernabeu first appeared on SpotiLEO.








