CAIRO: GOLIKIPA wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Hussein Masalanga amesema mchezo wao wa ufunguzi wa Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) dhidi ya Nigeria utakuwa mgumu kutokana na kiwango cha wachezaji wa timu hiyo wengi wanacheza soka la kulipwa Ulaya.
Akizungumza Leo katika maandalizi yao yanayoendelea nchini Misri, golikipa huyo amesema, “Tunakutana na mpinzani mgumu mwenye wachezaji wengi ‘professional. Hata hivyo, tuna imani kwa maandalizi mazuri chini ya Kocha Miguel Gamondi tutafanya vizuri.”
Amesema zaidi, “Tunaweza kufanya kitu ambacho wengi hawakitegemei kwa kuwa hata sisi tuna wachezaji wenye uzoefu na wanaocheza soka la ushindani nje ya nchi.”
Kwa mujibu wa golikipa huyo, maandalizi ya Stars yamekuwa na ushindani mkubwa ndani ya kikosi, jambo analosema limeongeza morali na kuimarisha umoja wa timu kuelekea mashindano hayo makubwa barani Afrika.
Tanzania itacheza mchezo wake wa ufunguzi dhidi ya Nigeria Desemba 23, kabla ya kukutana na Uganda katika michuano hiyo itakayofanyika nchini Morocco hivi karibuni.
The post Masalanga: Nigeria wagumu ila tutapambana first appeared on SpotiLEO.





