MADRID: KOCHA wa Real Madrid, Xabi Alonso, amesema wachezaji wake wanajitahidi kadiri ya uwezo wao kurejesha kiwango chao licha ya kuendelea kwa mwenendo mbaya baada ya kupoteza mabao 2-1 dhidi ya Manchester City katika Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano.
Alonso, aliyechukua timu hiyo mwezi Juni, yuko chini ya shinikizo baada ya kushinda mara mbili tu katika mechi nane kwenye mashindano yote. Madrid ililazimika kucheza na safu ya ulinzi iliyopangwa kwa dharura kufuatia majeraha ya Eder Militao, Trent Alexander-Arnold, Dani Carvajal, Dean Huijsen na mshambuliaji Kylian Mbappé kukosekana kutokana na majeraha.
“Tunakabiliana na majeraha, lakini wachezaji wangu wanatoa kila walichonacho, hivyo hakuna cha kulalamikia leo. Ninathamini sana mtazamo wao wa kila siku, na tunapaswa kuendelea kusonga mbele.” – Alonso alisema.

Madrid ilianza vizuri dhidi ya Manchester City na kuandika bao la kwanza kupitia Rodrygo bao lake la kwanza tangu Machi. Hata hivyo ndani ya dakika 10 mambo yakabadilika: Thibaut Courtois aliteleza katika kona na kumruhusu Nico O’Reilly kusawazisha, kabla Antonio Rüdiger kusababisha penalti kwa kumvuta Erling Haaland chini.
Kadri mchezo ulivyoendelea na Madrid kushindwa kutumia nafasi walizopata, mashabiki walianza kukosa uvumilivu na timu ikazomewa na kupigiwa miluzi walipotoka uwanjani.
Alonso amesema ni kawaida kwa mashabiki kuonesha hasira wanaposhindwa kupata matokeo chanya nyumbani, akiongeza kuwa yuko tayari kujikosoa kutokana na kile alichoita mchezo wa ovyo.
“Ukishindwa nyumbani, hali kama hii hutokea, lakini mara nyingi wamekuwa wakituunga mkono,” – aliongeza.
Real Madrid watakutana na Alaves kwenye LaLiga Jumapili.
The post “Tutajitahidi kurejesha kiwango chetu” – Alonso first appeared on SpotiLEO.







