MANCHESTER: MSHETANI wekundu Manchester United wameripoti hasara ya robo ya kwanza ya mwaka baada ya kukumbwa na upungufu wa mapato ya matangazo ya Televisheni na mauzo ya tiketi, kufuatia kukosa kushiriki mashindano ya Ulaya msimu huu.
Klabu hiyo ya Old Trafford imetangaza hasara ya pauni milioni 6.6 kwa robo iliyoishia Septemba 30, ikilinganishwa na faida ya pauni milioni 1.4 katika kipindi kama hicho mwaka jana. Mapato ya jumla yalishuka kwa asilimia 2, huku mishahara ya wachezaji na wafanyakazi ikipungua kwa asilimia 8.2 kufuatia hatua ya kupunguza ajira.
“Maamuzi magumu tuliyochukua katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita yamepunguza gharama kwa kiwango endelevu na kuboresha ufanisi wa uendeshaji, jambo litakalituwezesha kuisukuma klabu kuelekea mafanikio ya muda mrefu kimichezo na kibiashara,” – taarifa ya United imemnukuu Mtendaji Mkuu wake Omar Berrada
United ililazimika kuchukua hatua za kubana matumizi baada ya kurekodi hasara kwa miaka sita mfululizo, hali inayoonesha ugumu unaoikabili klabu hiyo yenye mataji 20 ya England, ambayo imekuwa ikisuasua ndani na nje ya uwanja.
Klabu hiyo imethibitisha makadirio yake ya mapato kwa mwaka wa fedha 2026 kubaki kati ya pauni milioni 640 hadi 660, pamoja na faida ya msingi ya kati ya pauni milioni 180 hadi 200.
Mmiliki mwenza Sir Jim Ratcliffe mwenye umiliki wa takribani asilimia 29 na anayesimamia masuala ya mpira tayari ameidhinisha ongezeko la bei za tiketi, licha ya klabu kutumia zaidi ya pauni milioni 230 kwenye dirisha la usajili la kiangazi na kutangaza mpango wa ujenzi wa uwanja mpya wa viti 100,000 utakaogharimu pauni bilioni 2.
Kutokuwepo kwa United kwenye mashindano ya Ulaya msimu huu kumeathiri vibaya mapato ya matangazo na kuongeza shinikizo la kifedha, huku mashabiki wakiongeza malalamiko wakati ambao timu imekuwa ikisuasua katika mashindano ya ndani.
The post United yaripoti tena hasara first appeared on SpotiLEO.





