OFISA Habari wa Yanga, Ali Kamwe, ameweka wazi kuwa si sahihi kwa klabu hiyo kuzungumzia mchezaji ambaye bado ana mkataba na timu nyingine, akisisitiza kuwa wanaheshimu taratibu za usajili pamoja na mikataba ya wachezaji.
Kauli hiyo imeibuka kufuatia gumzo linalomhusisha kiungo wa Simba, Elie Mpanzu, kufuatia taarifa zilizomnukuu Kamwe kana kwamba Yanga ina nia ya kumsajili mchezaji huyo katika dirisha dogo.
Kamwe amesema kwa sasa Yanga inaendelea kufanya kazi kwa kufuata mapendekezo ya Kocha Mkuu, Pedro Gocalves, ambaye tayari amekabidhi ripoti yake kwa uongozi ili kuboresha kikosi kuelekea mzunguko ujao wa ligi.
“Hatusajili kwa mihemuko. Kama kuna nafasi ipo basi tutaongeza mtu. Kuhusu Mpanzu, si busara kuzungumzia mchezaji mwenye mkataba. Ni mchezaji mzuri, lakini tunaheshimu mkataba wake,” amesema Kamwe.
Amesisitiza kuwa Yanga inafanya usajili kwa umakini mkubwa kwa kuangalia wachezaji ambao wamemaliza mikataba au wale waliobakiza miezi sita, ili kuhakikisha wanatoa mchango wa haraka ndani ya kikosi.
“Kama kuna mchezaji mzuri aliyebakiza miezi sita na timu yake imekubali ofa kipindi hiki cha dirisha dogo, basi tutapeleka pesa kwa ajili ya kufanya biashara,” amesema Kamwe.
The post YANGA YAFUNGUKA KUHUSU MPANZU appeared first on Soka La Bongo.





