UONGOZI wa klabu ya Simba umeamua kumuachia kocha mpya majukumu ya kupanga benchi lake la ufundi, hatua inayoweka sintofahamu juu ya hatma ya kocha msaidizi Selemani Matola ndani ya timu hiyo.
Maamuzi hayo yanakuja wakati Simba ikiwa kwenye mchakato wa kujipanga upya baada ya mabadiliko ya hivi karibuni katika benchi la ufundi.
Ripoti kutoka ndani ya klabu zinaeleza kuwa suala la Matola limekuwa likijadiliwa kwa muda, huku kukiwa na maoni tofauti kuhusu uwezekano wa kocha huyo kuendelea au kuondoka.
Uongozi umeamua kwamba ni kocha mpya pekee ndiye atakayekuwa na mamlaka ya mwisho katika kupanga ni nani atakayebaki kwenye benchi lake la ufundi.
Taarifa zinaeleza kuwa tathmini ya kina imefanywa kuhusu michezo iliyopita ya Simba, na sehemu ya maamuzi hayo ilikuwa kutathmini mchango wa Matola.
Awali kulikuwepo maamuzi ya kumwondoa, lakini uongozi umeamua kumwachia kocha mpya nafasi ya kuamua kama ataendelea kufanya kazi naye au vinginevyo.
Kwa sasa Simba ipo kwenye hatua za mwisho za kumpata kocha mpya atakayechukua nafasi ya Dimitar Pantev, aliyekuwa meneja wa timu hiyo kabla ya kuondolewa. Majina mbalimbali yamekuwa yakihusishwa lakini uongozi haujatangaza rasmi ni nani atakayerithi mikoba hiyo.
Chanzo kutoka ndani ya klabu kimeeleza kuwa kulikuwa na mvutano kuhusu suala la Matola, baadhi wakitaka aachwe, huku wengine wakiamini bado ana mchango kwa timu.
Hatimaye maamuzi yaliyopitishwa ni kumwachia kocha mpya uhuru kamili wa kuunda benchi lake la ufundi ili kuleta mabadiliko chanya.
Chanzo hicho kimeongeza kuwa uamuzi huo unalenga kuleta uwiano na utulivu ndani ya timu, kwani kocha mpya atahitaji uhuru kupanga watu anaowaamini kwa ajili ya kutekeleza falsafa zake za kiufundi.
“Hii inaonekana kuwa sehemu ya mpango mpana wa Simba kuhakikisha timu inarejea kwenye ubora wake wa ushindani,” amesema chanzo hicho.
Kwa upande mwingine, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amewatoa hofu mashabiki kwa kuwataka kuwa watulivu wakati mchakato wa kuimarisha benchi la ufundi ukiendelea.
Amesema uongozi uko makini kuhakikisha timu inapata mwelekeo sahihi kuelekea mechi zijazo na msimu ujao.
The post HATMA YA MATOLA MIKONONI MWA KOCHA MPYA appeared first on Soka La Bongo.







