MSHAMBULIAJI wa Wydad Casablanca, Mwalimu ambaye yupo kwa mkopo katika klabu ya Simba, ameongeza tabasamu kwa Watanzania baada ya kuthibitishwa rasmi kujiunga na kikosi cha Taifa Stars kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025.
Mwalimu awali hakujumuishwa katika kikosi cha mwisho kilichotangazwa siku chache zilizopita, hali iliyozua maswali miongoni mwa mashabiki wa soka nchini kuhusu hatma yake katika timu ya taifa.
Hata hivyo, benchi la ufundi la Taifa Stars limeamua kumrejesha mchezaji huyo kufuatia majeraha yaliyompata mshambuliaji Sopu, ambaye atalazimika kukosa mashindano hayo muhimu.
Hatua ya kumrejesha Mwalimu imekuja baada ya kukamilika kwa taratibu zote muhimu, ikiwemo kupatikana kwa viza yake kufuatia ziara yake katika ofisi ya balozi wa Misri, jambo lililoweka wazi njia yake ya kusafiri bila kikwazo.
Kwa mujibu wa taarifa, mchezaji huyo anatarajiwa kujiunga na kambi ya Taifa Stars jijini Misri, ambako timu inaendelea na maandalizi ya mwisho kuelekea AFCON 2025.
Ujio wa Mwalimu unaongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji ya Taifa Stars, huku uzoefu wake wa kimataifa ukitarajiwa kuisaidia timu katika mashindano hayo makubwa ya bara la Afrika.
Kwa ujumla, kurejea kwake kunachukuliwa kuwa habari njema kwa Tanzania, kwani kunazidi kuongeza matumaini ya kufanya vizuri katika AFCON 2025.
The post MWALIMU AWAPA TABASAMU WATANZIA NDANI YA STARS appeared first on Soka La Bongo.






