DAR ES SALAAM: MCHEZAJI wa mpira wa miguu, Stephen Aziz Ki, amesema kuwa taswira inayowafanya baadhi ya watu kumhukumu mke wake, mwanamitindo Hamisa Mobetto, si kielelezo halisi cha maisha yake ya ndani.
Aziz Ki amesema kuwa watu wengi humtazama Hamisa kupitia picha na maudhui yanayosambaa kwenye mitandao ya kijamii na kudhani kuwa ndivyo alivyo hata katika maisha ya kila siku, jambo ambalo amesema si la kweli.
Amefafanua kuwa taswira inayojitokeza mitandaoni inachangiwa zaidi na maisha ya umaarufu, huku akisisitiza kuwa katika maisha ya nyumbani, Hamisa ni mtu wa familia, mwenye upendo, mkarimu na mwenye hofu ya Mungu.
“Nina uhakika kwa asilimia 90 watu hawamjui vizuri mke wangu. Hawajui namna alivyo mkarimu wala jinsi anavyonipa sapoti kubwa katika maisha yangu,” amesema Aziz Ki.Ameongeza kuwa hata yeye mwenyewe alishangazwa na hulka halisi ya Hamisa walipoanza mahusiano, kwani hakutarajia kuona upande huo wa maisha yake binafsi.
“Hata mimi nilishtuka mwanzoni. Wakati tunaanza mahusiano, sikujua kama huyu ndiye Hamisa wa ndani ninayemjua, tofauti na yule Hamisa wa nje anayewaonesha watu,” amesema.
Aziz Ki amesema anaendelea kuthamini mchango na sapoti ya mke wake katika maisha yake ya kila siku, akiwataka watu kutambua kuwa maisha ya mitandao ya kijamii si kipimo sahihi cha utu wa mtu.
The post Aziz Ki: Wengi hawamjui Hamisa Mobetto wa ndani first appeared on SpotiLEO.






