DAR ES SALAAM: BONDIA Hamadi Furahisha amewaahidi Watanzania ushindi mnono dhidi ya mpinzani wake Hannock Phiri wa Malawi katika pambano litakalopigwa Desemba 26, 2025 Dar es Salaam.
Akizungumza mapema leo Yombo Dovya Dar es Salaam, Furahisha amesema anatambua ubora na hatari ya mpinzani wake ambaye ameshawapiga mabondia kadhaa wa Tanzania bila kupigwa, lakini safari hii ni tofauti kwani anakutana na bondia aliyedhamiria kumaliza kazi mbele ya mashabiki wake.
“Niko tayari kwa mapambano. Safari hii Hannock Phiri anakutana na mfupa wa sokwe, ushindi unabaki nyumbani.” Alisema.
Amesema maandalizi yake yamekamilika, yakiwa yamejikita katika mbinu, nguvu na kasi, akisisitiza kuwa Desemba 26 atahakikisha anamfurahisha Mmalawi huyo kwa kipigo cha kukumbukwa.
Kwa upande wao, wadau na mashabiki wa bondia huyo wameonesha imani kubwa kwake, wakisema Furahisha si bondia wa kawaida kwani hupiga huku akiwaburudisha mashabiki, jambo linalomfanya kuwa kipenzi cha wengi.
Mashabiki hao wamesisitiza kuwa Hannock Phiri anapaswa kujiandaa kisaikolojia kupokea kipigo anapokuja Tanzania, kwani Furahisha amedhamiria kuendeleza rekodi yake ya ushindi.
Mbali na pambano hilo, Watanzania wanatarajiwa kushuhudia mapambano makali mengine siku hiyo, yakiwemo pambano kati ya Hassan Mwakinyo dhidi ya Stanley Eribo kutoka Nigeria, Ally Ngwando dhidi ya Mussa Makuka, Issa Simba wa Kahama dhidi ya Wilson Phiri wa Malawi.
Kwa upande wa wanawake, Hidaya Zahoro wa Morogoro atakabiliana na Leila Macho wa Dar es Salaam, huku Debora Mwenda akizichapa na Mariam Dick wa Malawi.
The post Hamadi Furahisha atuma salamu kwa Mmalawi first appeared on SpotiLEO.







