OFISA Habari wa Yanga SC, Ali Kamwe, amesema kikosi cha timu hiyo kimerejea mazoezini baada ya mapumziko mafupi, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya awamu ya kwanza kuelekea michuano mbalimbali iliyopo mbele yao.
Kamwe amesema kurejea huko ni hatua muhimu kwa timu kuhakikisha inakuwa tayari mapema, hasa ikizingatiwa ushindani mkubwa uliopo katika Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na mashindano mengine ya ndani na kimataifa.
Ameeleza kuwa mazoezi hayo yameanza leo katika uwanja wa KMC Complex, yakihusisha wachezaji ambao hawapo kwenye majukumu ya timu zao za taifa zinazoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Kwa mujibu wa Kamwe, benchi la ufundi limeona ni muhimu kuanza mapema na kundi hilo la kwanza ili kuwapa maandalizi sahihi kabla ya kuunganishwa na wachezaji wengine watakaorejea kutoka majukumu ya kitaifa.
“Timu imerejea mazoezini leo chini ya kocha Patrick Mabedi, haya ni mazoezi ya awamu ya kwanza kabla ya wachezaji kupewa mapumziko mafupi kwa ajili ya sikukuu,” amesema Kamwe.
Ameongeza kuwa maandalizi hayo yanalenga kujenga mwendelezo wa ubora wa kikosi na kuepuka kusubiri muda wa mwisho, hali ambayo inaweza kuathiri utayari wa timu.
Kamwe amesisitiza kuwa Yanga haina muda wa kupoteza, akieleza kuwa ratiba ni ngumu na ushindani ni mkubwa, hivyo kila hatua ya maandalizi lazima ichukuliwe kwa umakini mkubwa ili kufikia malengo ya klabu msimu huu.
The post YANGA HATUNA MUDA WA KUPOTEZA, ALI KAMWE appeared first on Soka La Bongo.





