ONGOZI wa Yanga unaendelea na mazungumzo na klabu ya Sekhukhune United ya Afrika Kusini kuhusu hatma ya mshambuliaji Andy Boyeli, ambaye yupo kikosini hapo kwa mkopo.
Mazungumzo hayo yanalenga kusitisha mkataba wa mkopo wa mchezaji huyo mapema, kutokana na kushindwa kuendana na mahitaji ya kiufundi ya timu hiyo ya Jangwani.
Boyeli alijiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu huu kwa mkataba wa mkopo wa mwaka mmoja, wenye kipengele cha kumnunua moja kwa moja mwishoni mwa msimu wa 2025/26 endapo angeonyesha kiwango cha kuridhisha.
Katika makubaliano hayo, Yanga ilikuwa inalipa asilimia 50 ya mshahara wa mchezaji huyo huku sehemu iliyobaki ikigharamikiwa na Sekhukhune United.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Yanga, mabosi wa klabu hiyo wakishirikiana na kocha mkuu Pedro Goncalves wameanza kupiga hesabu kali za kuimarisha kikosi dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa mapema mwakani.
Hatua hiyo inalenga kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji ili kuifanya timu iwe na makali zaidi katika mapambano ya ndani na nje ya nchi.
Katika kuhakikisha eneo la mbele linapata ufanisi zaidi, Yanga imepiga hesabu za kumpiga chini Boyeli na kushusha mashine mpya ya mabao kutoka Angola.
Mshambuliaji huyo anayependekezwa ni Laurindo Dilson Maria Aurelio ‘Dupe’, ambaye pia ni mchezaji wa timu ya taifa ya Angola na anatajwa kuwa na uwezo mkubwa wa kufumania nyavu.
Chanzo cha kuaminika kutoka Yanga kililiambia Mwanaspoti kuwa, uongozi pamoja na benchi la ufundi wamekubaliana kuwa Boyeli hatakuwa sehemu ya mipango ya timu hiyo mara itakaporejea kutoka mapumziko.
Uamuzi huo umetokana na tathmini ya kiufundi iliyobaini kuwa timu ipo vizuri lakini inahitaji safu ya ushambuliaji iliyo makini zaidi ili kuleta ushindani na ushindi wa uhakika.
“Msimu huu Yanga ina washambuliaji watatu Prince Dube, Clement Mzize ambaye ni majeruhi na Boyeli, lakini safu hiyo imekuwa but kama matarajio ya uongozi na benchi la ufundi,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kiliongeza kuwa kwa sasa kinachofanyika ni kutafuta mbadala wa moja kwa moja dirisha lijalo, huku straika Depu akitajwa kuwa ndiye anayepigiwa hesabu kubwa ili kuongeza ushindani, kasi na ufanisi katika safu ya ushambuliaji wa Yanga kwa mwendelezo wa msimu.
The post appeared first on Soka La Bongo.







