MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, amewataka mashabiki na wanachama wa klabu hiyo kuwa makini na taarifa zinazotolewa na uongozi wa watani zao, Yanga, hususan zile zinazohusishwa na wachezaji wa Simba.
Ahmed amesema si mara ya kwanza kwa wachezaji wa Simba kuhusishwa na Yanga, akieleza kuwa kila msimu hali hiyo imekuwa ikijirudia kama sehemu ya mbinu za kuvuruga maandalizi ya klabu yao.
Kwa sasa, amesema majina ya Elie Mpanzu na Morice Abraham yamekuwa yakitajwa licha ya ukweli kwamba wote bado wana mikataba ya mwaka mmoja na Simba.
Amesema licha ya kutajwa mara kwa mara kwa wachezaji wao kutakiwa na Yanga, hakuna mchezaji wa Simba ambaye amewahi kukatisha mkataba wake ili kujiunga na mpinzani wao huyo wa jadi katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa Ahmed, lengo la taarifa hizo ni kutengeneza presha na kujaribu kuiondoa Simba katika mstari wa mipango yake ya kawaida, uongozi wa Simba umetambua mbinu hizo mapema na hautaruhusu kuingia katika mtego huo.
Ameongeza kuwa wachezaji wote wanaotajwa kuhitajika na klabu nyingine bado ni mali ya Simba hadi pale klabu itakapoamua vinginevyo, hakuna mchezaji anayeondoka bila ridhaa ya uongozi.
Ahmed amesisitiza kuwa kwa sasa hakuna mchezaji wa Simba ambaye anahitajika na klabu nyingine na kuruhusiwa kuondoka. Endapo mchezaji ataondoka, itakuwa ni baada ya Simba kuamua kuwa hana tena nafasi katika mipango ya timu.
Ahmed amewataka mashabiki wa Simba kuendelea kuwa watulivu na kuamini mwelekeo wa uongozi wao, akisisitiza kuwa klabu ipo kwenye reli yake sahihi na haitatetereka kutokana na kelele za nje.
The post SIMBA HATUTOKI KWENYE RELI KWA SABABU YAO appeared first on Soka La Bongo.






