MWENYEKITI a Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori, amesema bodi wanayoiongoza ipo imara na haiwezi kuyumbishwa na maneno au jitihada za watu wanaotaka kuwachonganisha na wanachama ili kuwatoa kwenye malengo ya kuijenga klabu hiyo ya Msimbazi.
Magori ameeleza kuwa lugha na mijadala inayolenga kuwagawanya wanachama na uongozi inapaswa kufikia mwisho, akisisitiza kuwa kwa sasa nguvu kubwa inaelekezwa katika kuimarisha mifumo ya klabu, ikiwemo maandalizi ya mfumo mpya wa kisasa wa utoaji wa kadi za wanachama.
Amesema dira ya bodi ni kuijenga Simba kuwa klabu yenye uwezo mkubwa kifedha na uongozi bora, akibainisha kuwa wanakwenda kutengeneza mifumo itakayoiwezesha klabu kuwa na mapato makubwa kuliko klabu nyingine zote nchini.
Akizungumzia upande wa kiufundi, Magori amesema kuyumba kwa timu kulitokana na mabadiliko ya benchi la ufundi mwanzoni mwa msimu, baada ya kocha aliyeanza na timu kuondoka na kocha aliyekuja baadaye kutokukubaliana na malengo ya klabu.
Ameongeza kuwa changamoto za majeruhi pia zimechangia hali hiyo, akieleza kuwa kwenye mechi ya Ngao ya Jamii beki muhimu wa kati aliumia, kisha mechi iliyofuata kipa namba moja naye akaumia, hali iliyoiathiri timu kwa kiasi kikubwa.
“Tulipo kuwa ugenini Mali, beki mwingine muhimu wa kati alipata majeraha, lakini badala ya kuelewa hali hiyo, maneno na kelele zimekuwa zikikuzwa bila kuangalia uhalisia, Simba imecheza mechi tano za ligi na kupoteza mchezo mmoja tu lakini kelele zimekuwa kubwa kana kwamba ni mwisho wa dunia,” amesema.
Magori, amesema kutofuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa si jambo walilolipenda wala walilokusudia, lakini si janga kama linavyoelezwa, akiwataka Wanasimba kuzungumzia mpira na kutoondolewa kwenye reli, huku akisisitiza kuwa bodi itaendelea kusimama imara bila kuyumbishwa na kelele za pembeni.
The post BODI BADO IPO IMARA HAIYUMBISHWI, MAGORI appeared first on Soka La Bongo.







