MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori, amesema kikao cha mwisho cha bodi kimepitisha rasmi katiba mpya ya klabu hiyo, ambayo sasa ipo katika hatua za mwisho za kusajiliwa, ikiwa ni hatua muhimu katika historia ya uendeshaji wa Wekundu wa Msimbazi.
Magori ameeleza kuwa mchakato wa mabadiliko ulioanza mwaka 2017 sasa unaelekea kufikia tamati baada ya takribani miaka minane ya changamoto, akibainisha kuwa mfumo wa uendeshaji wa Hybrid ulikuwa mgumu kutekelezwa na ulihitaji marekebisho ya kina ili kuendana na mazingira ya klabu.
Amesema Simba imefanikiwa kuvuka kipindi hicho kigumu, huku katiba mpya ikiweka misingi iliyo wazi ya majukumu kati ya mwekezaji na wanachama, pamoja na kurejesha zoezi la utoaji wa kadi za wanachama ambalo lilikuwa limesimamishwa kwa muda mrefu.
Katika hatua nyingine, Magori amesema klabu ina mpango wa kuanzisha kadi za kisasa za wanachama zitakazokuwa na matumizi mengi, akisisitiza kuwa mfumo huo hautakuwa na mfano wake nchini Tanzania na utaongeza ushiriki na manufaa kwa wanachama wa Simba.
Ameongeza kuwa baada ya mabadiliko hayo kukamilika, mwekezaji ataelekeza nguvu katika uwekezaji wa miundombinu, ikiwemo ujenzi wa uwanja wa kisasa wa mazoezi wenye hadhi ya nyota tano katika eneo la Bunju, hatua itakayoinua viwango vya maandalizi ya timu.
Magori amesema Simba ina bahati ya kuwa na mwekezaji ambaye pia ni mwanachama wa klabu hiyo, anayeelewa vyema falsafa na mahitaji ya Simba, huku akiteua viongozi wenye mapenzi ya dhati na maono ya kuisukuma klabu mbele.
Amesisitiza kuwa klabu iko kitu kimoja na kuwaomba mashabiki waendelee kuwa na imani, akibainisha kuwa mambo makubwa yanaendelea kupangwa chini ya kauli mbiu ya Nguvu Moja, huku Simba ikiendelea kudhihirisha ukubwa wake barani Afrika kwa kuwa ya pili kwa kufuatiliwa zaidi kwenye mitandao ya kijamii, nyuma ya Al Ahly.
The post KATIBA MPYA SIMBA YAPITA, UWANJA NYOTA TANO BUNJU appeared first on Soka La Bongo.







