LUSAIL: TIMU ya Taifa ya Morocco imetwaa ubingwa wa Kombe la Nchi za Kiarabu baada ya kuifunga Jordan mabao 3-2, kwa msaada wa mabao mawili ya Abderrazzaq Hamed Allah yaliyofuata bao la kusisimua la mbali la Oussama Tannane.
Morocco ilianza vyema mchezo huo kwa kupata bao mapema dakika ya nne, Tannane akifunga kwa shuti la kushangaza kutoka katikati ya uwanja lililomkuta mlinda mlango Yazeed Abulaila akiwa nje ya lango.
Jordan, ambao wanatarajiwa kushiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza mwaka 2026, walisawazisha kwa mabao mawili kipindi cha pili kupitia Ali Olwan, aliyefunga kwa kichwa dakika ya 48 na mkwaju wa penalti dakika ya 68.

Hata hivyo, Hamed Allah alirejesha matumaini ya Morocco kwa kufunga dakika tatu kabla ya filimbi ya mwisho na kusawazisha, kabla ya kuifungia timu yake bao la ushindi katika muda wa nyongeza kwa shuti la karibu na lango.
Ushindi huo umeipa Morocco taji jingine muhimu licha ya kukosa huduma za wachezaji kadhaa wanaocheza barani Ulaya, ikiwa ni maandalizi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
Morocco inaendelea kuandika historia katika soka la kimataifa. Ni taifa la kwanza kutoka Afrika na ulimwengu wa Kiarabu kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia, mafanikio yaliyopatikana Qatar miaka mitatu iliyopita walipowaondoa Hispania na Ureno kabla ya kufungwa na Ufaransa.
Mwezi Oktoba, Morocco pia ilitwaa ubingwa wa dunia kwa vijana chini ya miaka 20 baada ya kuifunga Argentina mabao 2-0 kwenye fainali, ikiwa ni taifa la kwanza la Kiarabu kufanikisha hilo. Timu ya chini ya miaka 17 ilifika robo fainali ya Kombe la Dunia, huku kikosi cha chini ya miaka 23 kikitwaa AFCON na kufuzu Michezo ya Olimpiki Paris 2024, ambako kilinyakua medali ya shaba.
Morocco ambao ni taifa mwenyeji wa AFCON, itakayofanyika kuanzia Desemba 21 hadi Januari 18. Itafungua michuano hiyo Jumapili hii dhidi ya Comoros mchezo utakaopigwa katika uwanja wa Prince Moulay Abdallah jijini Rabat majira ya saa 4 usiku Afrika mashariki
The post Morocco yaenda AFCON na kombe first appeared on SpotiLEO.






