LIVERPOOL: KOCHA wa Liverpool Arne Slot amesema hakuna tena mvutano kati yake na mshambuliaji wa klabu hiyo Mohamed Salah, akisisitiza kuwa wawili hao wamemaliza tofauti zao baada ya mshambuliaji huyo kuikosoa klabu hadharani hivi karibuni.
Akizungumza leo Ijumaa kuelekea mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Tottenham Hotspur utakaochezwa kesho Jumamosi, Slot amesema suala hilo limefungwa, huku Salah akiendelea kuwa sehemu muhimu ya kikosi.
“Nilisema wiki iliyopita, vitendo vinaongea zaidi ya maneno. Tumemalizana. Alikuwa kwenye kikosi na alikuwa mabadiliko ya kwanza niliyofanya. Sasa anaenda AFCON na atacheza mechi kubwa, hivyo ni haki umakini wote uelekezwe huko.” – amesema Slot.
Salah alikuwa mchezaji muhimu katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Brighton & Hove Albion wikiendi iliyopita, licha ya presha iliyokuwepo kabla ya mchezo huo kufuatia kauli zake kali dhidi ya klabu.

Kutegemea na safari ya Misri kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), Salah anaweza kukosa hadi mechi saba, kuanzia pambano la Jumamosi dhidi ya Spurs. Liverpool wapo nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi wakiwa na pointi 26, tofauti ya pointi 10 na vinara Arsenal, huku Tottenham wakiwa nafasi ya 11, pointi nne nyuma ya Liverpool.
Kwa upande wa majeruhi, Slot alithibitisha kuwa Cody Gakpo na Joe Gomez bado hawatakuwepo. Hata hivyo, Dominik Szoboszlai, aliyelazimika kutoka mwishoni mwa mchezo dhidi ya Brighton kutokana na jeraha la kifundo cha mguu, anaweza kurejea.
Liverpool, mabingwa watetezi, wameanza msimu kwa kusuasua lakini kwa sasa hawajapoteza katika mechi tano zilizopita kwenye mashindano yote, wakitarajia kuendeleza mwendo huo licha ya changamoto ya majeruhi na majukumu ya AFCON
The post Salah, Slot ‘wamemalizana’ first appeared on SpotiLEO.








