MWENYEKITI wa Klabu ya Simba, Murtaza Mangungu, ameweka wazi kuwa hakuna mgogoro wowote kati yake na mwekezaji wa klabu hiyo, Mohammed Dewji (Mo), akisisitiza kuwa mahusiano yao yako imara na mawasiliano yanaendelea kama kawaida.
Mangungu amesema kumekuwa na taarifa mbalimbali zinazosambazwa zikidai kuwepo kwa tofauti kati ya uongozi wa klabu na mwekezaji, lakini amezikanusha vikali akibainisha kuwa ni taarifa zisizo na ukweli wowote.
Ameeleza kuwa yeye pamoja na Rais wa heshima wana mawasiliano ya mara kwa mara, jambo linalothibitisha mshikamano uliopo katika uongozi wa juu wa klabu hiyo ya Msimbazi.
“Wanasema hakuna mgogoro kati ya upande wa klabu na mwekezaji, lakini mimi na Mwekezaji tunaongea kila mara. Kama ni Mo, mara ya mwisho niliongea naye jana saa nane,” amesema Mangungu.
Ameongeza kuwa hakuna jambo lolote linalofichwa ndani ya klabu, kwani masuala yote muhimu hujadiliwa kwa uwazi na kwa maslahi mapana ya Simba, huku mipango ya timu ikiendelea kama ilivyopangwa.
Mangungu amesisitiza kuwa endapo kutakuwa na taarifa muhimu kwa umma au mashabiki, uongozi hautasita kuziweka wazi, akiwataka mashabiki kupuuza uvumi na kuendelea kuiunga mkono timu yao.
The post SINA MGOGORO NA MWEKEZAJI, MANGUNGU appeared first on Soka La Bongo.








