LICHA ya mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize kuonekana akishiriki baadhi ya mazoezi ya timu, bado itachukua muda kabla ya nyota huyo kurejea rasmi uwanjani, huku ikielezwa kuwa Februari 2026 ndiyo mwezi unaotarajiwa kuanza kuonekana kwenye mechi za ushindani.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe amesema Mzize bado yuko mbali na kurejea katika kiwango cha kucheza mechi, licha ya kuonekana akifanya mazoezi ya gym sambamba na wachezaji wenzake kambini.
Kamwe ameeleza kuwa kwa sasa Mzize anaendelea na programu maalumu ya mazoezi chini ya usimamizi wa mtaalamu wa mazoezi ya viungo, hatua inayolenga kumfuatilia kwa karibu kabla ya kuanza kufanya mazoezi makali zaidi uwanjani.
Amefafanua kuwa baada ya kumaliza hatua ya mazoezi ya gym, Mzize atakabidhiwa kwa kocha wa viungo ili kuanza mazoezi ya kurejesha utimamu wa mwili, kabla ya kuanza mazoezi ya mpira kwa ukamilifu.
“Kwa Mzize tunatarajia mwanzoni mwa Februari aanze kuonekana uwanjani kutokana na jinsi ambavyo atakuwa amefikia kiwango kizuri cha utimamu wa mwili,” amesema Kamwe.
Kwa upande wa kiungo Attohoula Yao, Kamwe amesema mchezaji huyo tayari ameanza mazoezi ya utimamu wa mwili, jambo linaloashiria kurejea kwake kwenye mechi za ushindani mapema kulingana na tathmini ya benchi la ufundi.
“Kocha akiona anafaa na yupo kwenye mipango yake, Yao ataanza kucheza mechi za ushindani Januari hii,” amesema Kamwe, akibainisha kuwa uamuzi wa mwisho utabaki mikononi mwa kocha Pedro Goncalves.
The post UTETE WA YANGA MZIZE BADO SANA appeared first on Soka La Bongo.








