KLABU ya Stellenbosch FC imethibitisha rasmi kuondoka kwa Kocha Mkuu wake, Steve Barker, ambaye ameamua kuachia nafasi hiyo ili kuchukua changamoto mpya nje ya nchi, kujiunga na klabu ya Simba SC inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.
Barker alijiunga na Stellenbosch mwanzoni kama kocha msaidizi wa Sammy Troughton katika msimu wa kwanza wa klabu hiyo, kabla ya kuteuliwa kuwa Kocha Mkuu Julai 2017, uteuzi uliokuja kuwa sehemu muhimu ya safari ya kuijenga klabu hiyo hadi kuwa miongoni mwa timu zinazoheshimika nchini Afrika Kusini.
Katika kipindi chake cha karibu miaka tisa akiwa na Stellenbosch, Barker aliiongoza timu hiyo katika jumla ya mechi 309 kwenye mashindano mbalimbali, akifanikiwa kuipandisha daraja hadi Ligi Kuu baada ya kutwaa ubingwa wa National First Division msimu wa 2018/19.
Mbali na hilo, aliandika historia kwa kuifanya Stellenbosch kuwa timu ya kwanza kutwaa ubingwa wa Carling Knockout iliyoboreshwa mwaka 2023, hatua iliyothibitisha ukuaji na ushindani wa klabu hiyo chini ya uongozi wake wa kiufundi.
Pia, Barker aliiongoza Stellenbosch kucheza fainali za mfululizo za michuano ya MTN8 mwaka 2024 na 2025, sambamba na kufanikisha timu hiyo kufuzu mara mbili mfululizo kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup).
Akizungumza kuhusu uamuzi wake, Barker amesema ni maamuzi yenye hisia mchanganyiko lakini anaamini ni wakati sahihi kwa Stellenbosch kuingia katika zama mpya chini ya uongozi mwingine, huku akieleza kuwa kujiunga na moja ya klabu kubwa barani Afrika ni hatua muhimu katika kukuza ndoto na malengo yake binafsi ya ukocha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Stellenbosch FC, Rob Benadie, amemshukuru Barker kwa mchango wake mkubwa katika kuijenga klabu hiyo na kusema misingi aliyoweka itawezesha mabadiliko ya uongozi kufanyika kwa utulivu, huku akimtaja kama sehemu muhimu ya historia ya mafanikio ya Stellenbosch FC.
The post KOCHA BERKER APEWA BARAKA NA STELLENBOSCH appeared first on Soka La Bongo.







