DAR ES SALAAM:MSANII wa filamu za Kitanzania, John Elisha maarufu kama Boneka na anayefahamika pia kwa jina la Hamadi Kikala, amesema kuwa ndoto yake ya awali haikuwa uigizaji bali ilikuwa ni kuwa mchezaji wa mpira wa miguu wa kulipwa.
Akizungumza kuhusu safari ya maisha yake, Hamadi amesema kuwa aliwahi kuwa na ndoto kubwa ya kuitegemea soka kama chanzo chake kikuu cha maisha, kutokana na kipaji alichokuwa nacho katika mchezo huo.
Ameeleza kuwa aliwahi kujihusisha kikamilifu na masuala ya mpira wa miguu akiwa Butimba, ambapo alikuwa akifanya mazoezi na kushiriki michezo mbalimbali kabla ya ndoto hiyo kukumbwa na changamoto kubwa.
“Kwa bahati mbaya, mwaka 2014 nilipata jeraha baya la kuvunjika mguu baada ya kukanyagwa na mwenzangu katika eneo la kifundo cha mguu,” amesema Hamadi.
Jeraha hilo lilimlazimu kusitisha ndoto yake ya soka, hali iliyomfanya kubadili mwelekeo wa maisha na hatimaye kuingia kwenye tasnia ya uigizaji, ambako leo amejijengea jina kubwa.
Hata hivyo, Hamadi amefichua kuwa kabla ya jeraha hilo, alipata nafasi ya kucheza na baadhi ya wachezaji wakubwa waliokuja kucheza soka la kulipwa, akiwemo Dickson Ambundo, Yusuph Athumani, pamoja na wengine wengi.
The post Hamadi Kikala: Ndoto ya soka iliyoishia jukwaa la uigizaji first appeared on SpotiLEO.






