KOCHA mpya wa Klabu ya Simba, Steve Barker, anatarajiwa kutua nchini muda wowote kuanza maandalizi ya mashindano yanayoikabili timu hiyo, wakati kikosi cha Wekundu wa Msimbazi kinapangwa kuingia kambini rasmi Jumapili, Desemba 28.
Ujio wa Barker unakuja katika kipindi ambacho Simba inaelekeza nguvu zake kwenye mashindano mbalimbali ya ndani na kimataifa, huku benchi la ufundi likitarajiwa kuanza kazi mara moja kwa ajili ya kujenga kikosi imara na chenye ushindani.
Kocha huyo ataanza kazi rasmi kupitia michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambapo Simba itacheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Muembe Makumbi, Januari 3, katika Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar.
Barker anatarajiwa kuwasili nchini baada ya kumaliza mapumziko ya Sikukuu ya Krismasi akiwa na familia yake, ingawa taarifa zinaeleza kuwa ataingia nchini mwishoni mwa wiki hii tayari kuanza majukumu yake mapya.
Kocha huyo alitangazwa rasmi Desemba 19 kuchukua nafasi ya Dimitar Pantev, hatua iliyochukuliwa na uongozi wa Simba kama sehemu ya maboresho ya kiufundi kuelekea malengo ya klabu kwa msimu huu.
Katika ujio wake, Barker ataambatana na wasaidizi wanne, akiwamo Maahier Davids, ambaye ni mdogo wa aliyekuwa kocha wa Simba, Fadlu Davids, jambo linalotarajiwa kuleta mchanganyiko mpya wa uzoefu na mbinu benchi la ufundi.
Michuano ya Kombe la Mapinduzi inatajwa kuwa fursa muhimu kwa Barker kukitambua kwa kina kikosi cha Simba, kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa, ili kubaini maeneo yanayohitaji maboresho na kupanga mikakati ya baadaye
The post MUDA WOWOTE BARKER KUTUA NCHINI appeared first on Soka La Bongo.






