WAKATI kikosi cha Yanga kikiwa kwenye mapumziko ya mafupi, beki wa timu hiyo, Attohoula Yao, ametumia muda huo kuendelea kujifua ili kurejesha kiwango chake na kumshawishi kocha Pedro Goncalves kumpa nafasi ndani ya kikosi cha kwanza.
Yao amekuwa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu baada ya kusumbuliwa na majeraha yaliyomuweka pembeni kwa muda mrefu, hali iliyomfanya kukosa nafasi ya kucheza mechi za ushindani akiwa na timu hiyo.
Baada ya kupona, beki huyo ameanza kurejea taratibu katika hali yake ya kawaida na tayari ameungana na wachezaji wenzake katika kambi ya timu, akionesha nia ya kurejea katika ushindani wa ndani ya kikosi.
Katika kipindi cha mapumziko, Yao ameonekana kutumia muda mwingi kufanya mazoezi binafsi ya Gym chini ya uangalizi wa mtaalamu maalum, akilenga kuimarisha nguvu za mwili, stamina na utimamu wake kwa ujumla.
Hatua hiyo inaonekana kuwa sehemu ya mkakati wa nyota huyo kujijengea imani kwa benchi la ufundi, hasa kwa kocha Pedro, ili kuonesha kuwa yuko tayari kushindana na mabeki wengine waliopo kikosini.
Jitihada za Yao zinaelezwa kuwa zimeongeza ushindani ndani ya timu, jambo linalotarajiwa kuipa Yanga faida katika mechi zijazo kutokana na uwepo wa wachezaji wengi wenye ushindani wa nafasi.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, beki huyo tayari ameungana na wachezaji wenzake na ameanza kushiriki katika michezo ya ushindani, ishara kuwa yuko tayari kurejea kikamilifu uwanjani.
The post YAO KOUASSI MTIHANI MZITO KWA PEDRO appeared first on Soka La Bongo.






