NA DENIS MLOWE, IRINGA
UWANJA wa Samora ulibubujika na shamrashamra baada ya Meya wa Manispaa ya Iringa, Ibrahim Ngwada, kuzindua rasmi Bonanza la Mbunge Ngajilo, tukio ambalo limewaleta pamoja mamia ya wakazi wa manispaa hiyo kwa lengo la kuhamasisha michezo, afya na umoja katika jamii.
Bonanza hilo limekuwa miongoni mwa matukio makubwa ya michezo kuwahi kufanyika katika manispaa kwa kipindi cha miaka ya karibuni ikiwa na michezo zaidi ya 7 kwa wakati mmoja na kufanyika kwa siku 5 mfufulizo.
Katika bonanza hilo limezinduliwa likiwa na michezo ya zaidi ya 13 ikiwemo Mpira wa miguu , Netball,Rede ,Jogging ,Bao / Solo Draft , Baiskeli ,Muziki na dansi , Mashindano ya kula & kunywa ,Kuvuta kamba ,Stand-up comedy,Michezo ya watoto na Mbio za magunia
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Meya Ngwada alisema bonanza hilo ni ishara ya mwelekeo mpya wa viongozi wa Iringa katika kuwashirikisha wananchi kupitia shughuli za kijamii na michezo.
“Hii ni siku ya kihistoria. Tumeamua kutumia michezo kama nguzo ya kuwaleta watu wetu pamoja na kuhamasisha maisha yenye afya. Bonanza hili linafungua ukurasa mpya katika ajenda yetu ya kuendeleza vipaji,” alisema.
Ngwada aliongeza kuwa Manispaa ya Iringa inafanya juhudi za kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya michezo, akisisitiza kuwa maendeleo ya vijana hayawezi kutenganishwa na uwepo wa fursa sahihi. “Tukiwekeza kwenye viwanja, klabu za vijana na mashindano kama haya, tunawapa vijana wetu nafasi ya kujenga nidhamu, kujiamini na kuonesha vipaji vinavyoweza kuwafungulia milango ya mafanikio,” aliongeza.
Bonanza hilo, ambalo limejumuisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mbio fupi, kuvuta kamba, netiboli na michezo ya wanawake, limeonekana kuvutia washiriki wa rika tofauti, wakiwemo wanafunzi, wafanyabiashara, vikundi vya vijana na watumishi wa taasisi mbalimbali. Uwanja wa Samora ulijaa hamasa ya burudani, na mashabiki walioufurahia mpangilio wa siku nzima.
Akizungumza kwa niaba ya Mbunge Ngajilo, Katibu wake, Yahaya Mpelembwa, alisema bonanza hilo limeandaliwa kwa lengo mahsusi la kuzalisha vipaji na kuwakutanisha wananchi katika mazingira yenye tija. “Mheshimiwa Mbunge anaamini kuwa mabadiliko ya kweli katika jamii yanaanza na kujenga msingi imara kwa vijana. Bonanza hili si tu burudani, bali ni jukwaa la kugundua vipaji ambavyo vinaweza kuja kuipeperusha bendera ya Iringa kitaifa,” alisema.
Mpelembwa alisisitiza kuwa Mbunge Ngajilo ataendelea kuwa mdau mkubwa wa michezo, hasa katika kutoa vifaa, kuandaa mashindano na kuwaunganisha wadau wanaoweza kusaidia kuibua vipaji. “Vijana wa Iringa wanahitaji kuaminiwa. Mbunge amejipanga kuongeza mashindano ya mara kwa mara na kuanzisha programu za mafunzo kwa wanamichezo,” aliongeza
Wakazi waliohudhuria uzinduzi huo walisema bonanza hilo limetoa fursa adimu ya kukutana na kufanya mazoezi.









