*Wasema Madhabahu ni ya Injili, si majibizano
Na Mwandishi Wetu
Baadhi ya waumini wa Kanisa Katoliki Mkoa wa Dar es Salaam wametoa wito wa kurejeshwa kwa utamaduni wa mazungumzo ya ndani, heshima na umoja kanisani, wakisisitiza kuwa madhabahu inapaswa kutumika kuhubiri Injili ya upendo, si kuwa jukwaa la majibizano au hukumu.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, waumini hao wamesema kuwa kanisa linapaswa kuendeshwa kwa misingi ya maandiko matakatifu, ambapo changamoto zozote zinapaswa kushughulikiwa kwa busara, faragha na kwa kuzingatia taratibu za kikanisa.
Miongoni mwa waumini hao ni Mackdeo Shilinde na Gerald Abel, ambao wamesisitiza kuwa matumizi ya lugha kali kutoka madhabauni yanakiuka dhamira ya msingi ya mimbari, ambayo imekusudiwa kuunganisha waumini, kuwafariji na kuwajenga kiroho.
Wamesema kuwa iwapo kulikuwepo hoja au malalamiko yaliyowasilishwa kwa mamlaka za juu za Kanisa, njia sahihi ingekuwa ni kuyashughulikia kwa vikao na taratibu za ndani, badala ya kuyaweka wazi hadharani kupitia mahubiri.
Katika msimamo wao, waumini hao wamesisitiza kuwa Kanisa si mali ya Askofu au Padri mmoja, bali ni jumuiya pana ya waumini wote. Wamesema kauli au vitendo vinavyoweza kuwakwaza waumini vinapaswa kuepukwa kwa kuwa vinadhoofisha mshikamano wa kanisa.
Shilinde amesema kuwa lugha ya dharau au matusi, ikiwemo maneno yanayodhalilisha utu wa waumini, hayana nafasi katika mahubiri ya kanisa na yanapingana moja kwa moja na mafundisho ya Biblia yanayosisitiza upole, unyenyekevu na neema katika mawasiliano.
Wameongeza kuwa kauli za kauli za Askofu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Jude Thaddeus Rawai’chi ya kusema lofa”, “mpumbavu”, “njaa njaa”, “msaliti” kwa kutumia madhabahu haikuwa sawa.
Waumini hao wamenukuu maandiko mbalimbali ya Biblia yanayokataza hukumu na udhalilishaji, yakiwemo “Msihukumu, msije mkahukumiwa” (Mathayo 7:1), wakisisitiza kuwa kiongozi wa kiroho anatakiwa kuwa mfano wa hekima na uvumilivu.
Kwa mujibu wao, mimbari imewekwa mahsusi kwa ajili ya kuimarisha imani na umoja wa waumini, si kuibua migawanyiko. Wamesema Kanisa linapaswa kuwa kimbilio la watu wote bila kujali mitazamo yao, na si eneo la kuwatenga au kuwanyanyapaa.
Aidha, wamesema hoja zilizowasilishwa katika barua ya waumini kwenda kwa mamlaka za juu za Kanisa zilihitaji kujibiwa kwa hoja na uchunguzi wa kikanisa, badala ya kujibiwa kwa kauli zinazoweza kuwakwaza waumini wengi.
Katika hitimisho lao, Shilinde na Abel wamesisitiza kuwa Kanisa Katoliki linapaswa kubaki nje ya siasa za vyama, huku viongozi wa dini wakitakiwa kuwa waunganisha wa waumini na Taifa kwa ujumla.
“Padri si Kanisa, Askofu si Kanisa; Kanisa ni waumini,” wamesema, wakiongeza kuwa Kanisa linapaswa kuendelea kuwa nyumba ya sala, amani na maridhiano kwa wote.





