UONGOZI wa Klabu ya Yanga unaendelea kuonyesha nia ya kufanya usajili wa kiwango cha juu kuelekea dirisha dogo la usajili , huku ukiwa unahusishwa na mpango wa kunasa saini ya mshambuliaji wa Timu ya Taifa ya Angola, Gelson Dala.
Dala, ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya Al-Wakra inayoshiriki Ligi Kuu ya Qatar, alijiunga na timu hiyo akitokea Rio Ave ya Ureno. Mshambuliaji huyo amekuwa akionyesha kiwango kizuri ndani na nje ya nchi, jambo lililovutia macho ya viongozi wa Yanga.
Katika michuano ya AFCON inayoendelea nchini Morocco, Dala ameendelea kuthibitisha ubora wake baada ya kufunga bao katika mchezo dhidi ya Zimbabwe, hatua iliyozidi kuimarisha nafasi yake kama mmoja wa washambuliaji hatari wa Angola.
Inaelezwa kuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, ndiye anayesisitiza kupatikana kwa saini ya Dala, akiamini ni mchezaji anayelingana na falsafa yake ya soka na mahitaji ya kikosi anachokijenga kwa ajili ya mashindano ya ndani na ya kimataifa.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya klabu hiyo kimeeleza kuwa uongozi wa Yanga umejipanga kufanya usajili kwa kuzingatia mapendekezo ya benchi la ufundi, lengo likiwa ni kuongeza nguvu kwenye kikosi ili kiwe imara zaidi msimu ujao.
“Hersi yupo Morocco na amepata nafasi ya kuwaona wachezaji mbalimbali katika AFCON. Ameweza kubaini wale wanaoweza kutusaidia, akiwemo Gelson Dala ambaye amekuwa akifanya vizuri,” kilisema chanzo hicho.
Nyota huyo wa Angola pia amewahi kupitia klabu kubwa ya Sporting CP ya Ureno. Endapo Yanga itafanikiwa kupata saini yake, Dala anatarajiwa kuongeza ushindani mkubwa katika safu ya ushambuliaji, akiungana na Prince Dube pamoja na Clement Mzize, jambo litakaloongeza makali ya kikosi cha Wananchi .
The post YANGA HAINA MASIHARA KWENYE USAJILI appeared first on Soka La Bongo.





