NA DENIS MLOWE, IRINGA
KATIBU wa Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Yahaya Mpelembwa ameeleza kwa kina malengo na umuhimu wa bonanza la michezo la siku tano linaloendelea katika uwanja wa Samora.
Akizungumza na Full Shangwe Blog. Mpelembwa alisema kuwa bonanza hilo, lengo kuu ni kuimarisha umoja, kukuza vipaji na kuhamasisha ushiriki wa vijana katika shughuli chanya, hususan michezo ambayo imekuwa ikiwakutanisha wananchi kutoka maeneo tofauti.
Alibainisha kuwa michezo si burudani pekee, bali ni njia muhimu ya kujenga afya ya mwili na akili, kuimarisha nidhamu, pamoja na kuwaunganisha wananchi bila kujali itikadi za kisiasa, dini au hali zao za kijamii.
“Bonanza hili limekuja wakati muafaka ambapo tunataka kuona vijana wakitumia muda wao katika shughuli zenye tija. Kupitia michezo tunajenga umoja, tunatambua vipaji, na tunatoa nafasi kwa vijana kuonekana na kuchukuliwa na timu mbalimbali,” alisema Katibu huyo.
Aidha, aliongeza kuwa bonanza hilo linaloendelea kwa muda wa siku tano linajumuisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, mbio fupi, kuvuta kamba, rede na michezo ya jadi kama bao ili kuhakikisha kundi kubwa la washiriki linanufaika.
Kwa mujibu wa Katibu huyo, mpango huo pia umebeba ajenda ya maendeleo kupitia michezo alisema kuwa ushiriki mkubwa wa vijana katika bonanza hilo ni ishara ya ari mpya ya maendeleo katika jimbo hilo, na kwamba ofisi ya mbunge itaendelea kuunga mkono programu zote zinazolenga kuinua ustawi wa jamii.
Alisema kuwa mbunge mwenyewe amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha vijana wanapata fursa za kuonyesha uwezo wao, na bonanza hilo ni sehemu ya mkakati mpana wa kuandaa vipaji vitakavyoweza kushindana ndani na nje ya mkoa.
Wananchi waliohudhuria uzinduzi wa bonanza hilo wamepongeza juhudi hizo, wakisema kuwa ni hatua muhimu katika kupunguza changamoto za ajira, kuimarisha mahusiano ya kijamii na kutoa burudani ya afya ndani ya jamii.
Bonanza hilo linatarajiwa kufikia kilele chake siku ya Disemba 31 ambapo zawadi mbalimbali zitatolewa kwa washindi zenye thamani ya milioni 3.7
Nao baadhi ya wadau wa masuala ya michezo katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa wameiomba Serikali kuona umuhimu wa kuwekeza nguvu zaidi katika mchezo wa mpira wa pete, kama inavyofanyika kwa mchezo wa soka, ili kupanua wigo wa upatikanaji wa fursa kwa vijana wa kike kuonesha uwezo na vipaji walivyonavyo.
Wamesema uwekezaji huo utasaidia kuinua mchezo huo, kuongeza ushiriki wa wasichana na wanawake, na hatimaye kutoa nafasi kwa vijana hao kujiajiri na kujipatia kipato kupitia michezo.
Mratibu wa mchezo wa mpira wa pete katika muendelezo wa Ngajilo Bonanza 2025, Samweli Komba, amesema kuwa kwa sasa mchezo wa netiboli umepuuzwa kwa kiasi kikubwa, hali inayosababisha vipaji vya watoto wa kike kukosa kipaumbele na fursa za kuendelezwa ipasavyo.
Ameongeza kuwa endapo jitihada za makusudi hazitachukuliwa, vipaji vingi vya wasichana vitaendelea kupotea licha ya kuwa na uwezo mkubwa wa kuibua mafanikio kupitia michezo.






