KLABU ya Yanga imemtambulisha rasmi kiungo Mohammed Damaro kuwa mchezaji wake mpya, akitia saini mkataba utakaomuweka ndani ya kikosi hicho hadi mwisho wa msimu wa 2025/2026.
Usajili wa Damaro umefanyika kupitia makubaliano ya kubadilishana wachezaji kati ya Yanga na Singida Black Stars, ambapo Damaro ametua Jangwani huku beki Balla Conte akielekea kuitumikia Singida Black Stars.
Hatua hiyo inaonyesha wazi dhamira ya uongozi wa Yanga kuendelea kuimarisha kikosi chake kuelekea mashindano mbalimbali ya ndani na kimataifa, huku wakilenga kuongeza ushindani na ubora katika kila idara ya timu.
Utambulisho wa kiungo huyo umeambatana na shangwe kubwa kutoka kwa mashabiki wa Yanga, wameonesha matumaini makubwa juu ya mchango wa Damaro katika kikosi cha Wananchi msimu ujao.
Damaro anajiunga na Yanga akitokea Singida Black Stars ambako alikuwa mhimili muhimu wa timu hiyo, akionesha uwezo mkubwa wa kukaba, kupiga pasi sahihi na kuunganisha safu ya ulinzi na ushambuliaji. Uwezo huo ulimfanya kuwa miongoni mwa wachezaji waliokuwa wakihitajika zaidi katika dirisha la usajili.
Uongozi wa Yanga umeeleza kuwa kumsajili Damaro ni sehemu ya mkakati wa kuongeza ushindani wa ndani ya kikosi na kuleta uwiano mzuri kati ya wachezaji wenye uzoefu na vipaji vipya, wakiamini ataongeza nguvu kubwa katika safu ya kiungo.
Kwa upande wake, Damaro ameonesha furaha kubwa kujiunga na Yanga, akieleza kuwa ni heshima kwake kuvaa jezi ya klabu hiyo kongwe na yenye historia kubwa katika soka la Tanzania.
Kwa ujio wa Damaro, Yanga inaendelea kudhihirisha nia yake ya kweli ya kupambana vikali katika msimu wa 2025/2026, huku Wananchi wakiingia msimu huo wakiwa na matumaini mapya ya kuona kikosi chao kikifanya vizuri na kufikia malengo waliyojiwekea.
The post JANGWANI WATAMBULISHA SILAHA YAO MPYA appeared first on Soka La Bongo.





