BREMEN:TAARIFA zinaeleza kuwa Werder Bremen na Bayer Leverkusen wamekubaliana kuwa mshambuliaji wa Nigeria, Victor Boniface, atalazimika kufanyiwa upasuaji mwingine wa goti, hali inayoweka hatarini mustakabali wa maisha yake ya soka.
Boniface, mwenye umri wa miaka 25, ameripotiwa kuwa na uharibifu mkubwa wa goti ambao hauwezi kurekebishwa kirahisi, jambo lililowafanya madaktari kupendekeza afanyiwe operesheni nyingine. Kwa mujibu wa taarifa, jeraha hilo ni zito kiasi kwamba linaweza kuhitimisha kabisa kazi yake ya kucheza mpira wa miguu.
Kutokana na hali hiyo, nyota huyo wa Leverkusen anatajwa kuwa anafikiria kwa umakini kustaafu soka mapema, licha ya kuwa bado yuko kwenye umri mdogo(miaka 25 tu) na akiwa kileleni mwa ndoto za wachezaji wengi.
Ikumbukwe kuwa msimu wa joto uliopita, AC Milan walikuwa karibu kumsajili Boniface, lakini dili hilo likavunjika baada ya mshambuliaji huyo kushindwa vipimo vya afya kutokana na matatizo hayo ya goti.
Kwa sasa, macho yote yanaelekezwa kwenye uamuzi wa mwisho wa Boniface, huku mashabiki na wadau wa soka wakisubiri kwa huzuni kuona hatma ya mchezaji ambaye wengi waliona ana mustakabali mkubwa barani Ulaya.
The post Goti lamuweka Victor Boniface matatani first appeared on SpotiLEO.





